SUAMEDIA

Siku 14 za Usajili zatolewa SUA kwa waliochelewa kufanya Udahili ili Kujisajili

Na:Winfrida Nicolaus

Kupitia Usajili wa wanafunzi kwa Mwaka wa Masomo 2022/2023 unaoendelea kufanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam imetoa nafasi ndani ya siku 14 za Usajili kwa wale ambao wamechelewa kufanya udahili ndani ya siku hizo ili waweze kusajiliwa kwa ajili ya kuanza Muhula mpya wa masomo.

Hayo yamebainishwa Oktoba 25, 2022 mkoani Morogoro na Bw. Peter Lubuva Mresa, Afisa Udahili katika Kurugenzi hiyo wakati akifanya mazungumzo kwenye kipindi cha Mchakamchaka kinachorushwa hewani na SUA FM.

Amesema zoezi la Usajili wa Wanafunzi wa Shahada za Juu limeanza tarehe 24 Octoba, 2022 na litachukua muda wa siku 14 hivyo kupitia zoezi hilo wametoa nafasi kwa wale waliochelewa Udahili kutumia siku hizo kwa ajili ya kufanya udahili ambao unafanywa kwa njia ya mtandao ambapo ndani ya siku moja au mbili mtu anaweza akadahiliwa na kupata barua yake ya Udahili na kwenda Chuoni kufanyiwa Usajili ili kuanza masomo.

“Dirisha la Usajili limefunguliwa rasmi tarehe 24/10/2022 kwa wanafunzi wote wanaosoma Shahada za Uzamili au Uzamivu na dirisha hili la usajili litakuwa wazi kwa muda wa siku 14 hivyo wanafunzi wanapaswa kujisajili katika kipindi hicho na hata kwa wale waliochelewa udahili bado kuna nafasi chache zimetolewa hivyo wanaweza kutumia fursa hii kwa kipindi hiki cha Usajili kuweza kudahiliwa na moja kwa moja kusajiliwa”, amesema Bw. Lubuva

Aidha Afisa Udahili huyo amevitaja vitu vya msingi vya kuzingatia kwa wanafunzi wanaoenda kufanyiwa usajili kuwa ni barua ya kuitwa Chuoni, nakala halisi ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vyake vyote vya masomo ikiwa ni pamoja na hati za matokeo, nakala zilizothibitishwa za vyeti vyote, kwa waajiriwa aje na barua kutoka kwa mwajiri wake wa sasa, bima ya Afya pamoja na Ada.

Vilevile kwa wanafunzi wageni wanaotoka nje ya nchi wanatakiwa wawe na nakala ya hati ya kusafiria ambayo inaonesha taarifa zake zote za msingi na kwa wale ambao wanajilipia wanatakiwa kuandaa malipo kwa kuweka kwenye simu zao za mikononi na kwenye akaunti zao za benki ili watakapopata nambari ya uthibiti (Control Number) waweze kulipia.

Ameongeza kuwa kwa Mwaka wa Masoma 2022/2023 kuna punguzo la Ada ambalo ni nafuu na rafiki kwa wanafunzi wa Shahada za Juu hivyo mwanafunzi anaruhusiwa kulipa kwa awamu nne au kama ana uwezo kulipa kwa mkupuo,  vile vile kupitia Ada mpya kwa mwaka huu imetoa unafuu kwa watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kulipa kama watanzania. 













 


Post a Comment

0 Comments