Na: Ayoub Mwigune
Wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza wa Shahada za Awali katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kukamilisha hatua zote zinazohitajika ili kukamilisha Usajili kwa wakati ndani ya siku saba za usajili zilizopangwa kuanzia 24 Oktoba, 2022 kwa ajili ya kuanza masomo kwa muhula mpya wa masomo kwa mwaka unaoanza Oktoba 31, 2022.
Amebainisha hayo Mkurugenzi wa
Shahada za Awali Dkt. Nyambilila Amuri wakati akizungumza na SUAMEDIA Oktoba
25, 2022 kuhusiana na vitu vya kuzingatia ili kukamilisha Usajili wa wanafunzi
wa mwaka wa kwanza kwa Shahaza za Awali unaoendelea chuoni hapo.
Amesema mwamko wa wanafunzi
katika zoezi la Usajili litakalochukua muda wa siku saba ambalo lilianza Oktoba
24, 2022 ni mzuri ukilinganisha na
kipindi kilichopita kwani wanafunzi wameripoti kwa wakati hata hivyo Usajili
bado unaendelea kwa kuwa si wote waliodahiliwa wamemaliza usajili ndio maana
wanafunzi wanasisitizwa kukamilisha hatua zote zinazohitajika ili kukamilisha
usajili kwa wakati.
Dkt. Nyambilila amesema ni muhimu
mwanafunzi kuzingatia muda uliopangwa kwa ajili ya Usajili kwa kuwa akikosa
zoezi hilo atashindwa kufahamu vitu vya msingi ikiwemo kufahamu mazingira ya
Chuo, kupata mafunzo mbalimbali
yatakayotolewa na Wakuu wa Idara mfano kuhusu Afya, kujua jinsi ya kujitambua
ili kuweza kuishi maisha ya ushindi pindi wawapo chuoni.
“Kwa wanafunzi ambao wameshafika
Chuoni lakini bado hawajasajiliwa wanaweza kuendelea kujisajili kwa kuingia
kwenye akaunti zao ambazo wameombea maombi watakutana na kitufe cha register
atabonyeza hapo na kuhakiki taarifa zake zote hata zile za ziada na kuendelea
na hatua zitakazofuata ili aweze kukamilisha usajili,” amesema Dkt. Nyambilila.
Kwa upande wake Datius Raphael
mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza SUA amesema Chuo kimejipanga vizuri kuanzia upande
wa mapokezi kwani wanafunzi wamepokewa vizuri na wamefurahia huduma hiyo.
Akizungumzia Usajili kwa njia ya
mtandao mwanafunzi huyo amesema njia hiyo imerahisisha kazi na kufanya
wanafunzi kusajiliwa kwa wakati hivyo kuepusha msongamano.
0 Comments