SUAMEDIA

Waajiriwa wapya SUA watakiwa kuwa waadilifu na wawajibikaji


Na:Winfrida Nicolaus

Waajiriwa Wapya wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wametakiwa kuwa waadilifu na wawajibikaji katika kutekeleza majukumu yao ya kazi kama watumishi wa Umma ili kukisaidia Chuo katika kutimiza malengo yake kama Taasisi na Taifa kwa ujumla.

Amebainisha hayo Bi. Hilda Chigudulu, Afisa Utumishi Mwandamizi katika Chuo hicho wakati wa zoezi la kuwapokea waajiriwa wapya wanaojiunga na Chuo cha Sokoine cha Kilimo SUA ambapo amesema lengo la mapokezi hayo ni kuwafahamisha taratibu mbalimbali wanazotakiwa kuzifuata kama watumishi wa umma ili wanapoenda kuanza majukumu yao waende kutumika wakiwa wamefahamu nini majukumu yao na nini Chuo kinatarajia kutoka kwao.

Amesema katika kutekeleza majukumu yao kama watumishi wa Umma uwajibikaji ni jambo la kuzingatia hivyo katika kuhakikisha wanatengeneza taifa la watu wawajibikaji wanapaswa kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao hasa kwa watu wanaowatumikia vilevile kuheshimu mamlaka husika.

‘‘Ukiwa kama mtumishi wa Umma unatakiwa kufuata taratibu zote za utumishi wa umma hasa katika kufahamu yale unayotakiwa kufuata ukiwa kama mtumishi wa Umma na yale yasiyotakiwa kufuatwa zaidi Nidhamu ikiwa na maana ya kuheshimu Mamlaka husika, Mawasiliano mazuri baina ya wafanyakazi na hasa kwa watu unaowatumikia lakini pia kuhakikisha unatumia vizuri mitandao kwa faida yako wenyewe zaidi Muajiri wako ’’, amesema Hilda Chigudulu

Kwa upande wake Bw. Agustin Matondo Mwenyekiti wa Kamati ya Taaluma SUASA amesema wamefurahia kuongeza idadi ya wanachama katika Chama chao cha Wanataaluma vilevile katika kuanza safari ya kiutumishi amewasisitiza kuendana na maadili kama watumishi wa kada maalum ya Wanataaluma katika kufanikisha malengo ya Taasisi.

Naye Jenipher Tairo mmoja kati ya waajiriwa wapya katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo amesema kwa yale ambayo wameyapata katika mapokezi yao wanaamini yatawajenga zaidi na kuwawezesha kukisaidia chuo katika kufikia malengo yake ambayo wamejiwekea na kukifanya kuwa Chuo bora cha Kilimo Tanzania na Duniani kwa ujumla.

Mbonea Mweta ambaye pia ni Mwajiriwa mpya chuoni hapo amesema anafuraha kubwa kujiunga na jamii ya wasomi wa SUA lakini pia anaimani kwa niaba ya wenzake waliopata nafasi chuoni hapo wataleta maendeleo na matokeo chanya kwa kuzingatia Kanuni, Miongozo, Sheria pamoja na Taratibu mbalimbali ambazo zinahusiana na utumishi wa Umma lengo likiwa kuisukuma Tanzania kimaendeleo.







Post a Comment

0 Comments