Na:Winfrida Nicolaus
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA katika kuunga mkono jitihada za Serikari za kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la watoto wa kike kusoma masomo ya Sayansi na kupitia wito wa Rais Samia Suluhu Hassani za kuwataka wasichana kuchangamkia fursa zilizopo pamoja na kuwapa kipaumbele kwenye nafasi mbalimbali ikiwemo Uongozi kimewataka wasichana kuongeza jitihada katika masomo yao hasa katika masomo ya Sayansi kwa maendeleo ya nchi.
Amebainisha hayo Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akizungumza na Wanafunzi wa kike kutoka shule nne za sekondari za mikoa minne tofauti ambayo ni Iringa, Dodoma, Dar Es Salaam na Pwani ambao wameungana na wanafunzi wenyeji wa Mkoa wa Morogoro kutoka Shule ya Sekondari ya SEGA wakati walipofanya Ziara chuoni hapo kwa lengo la kujifunza na kuona Programu ambazo zinafanyika chuoni hapo.
Amesema lengo la Chuo kwa miaka minne ijayo ni kuhakikisha wanafikia asilimia 50 ya wanafunzi wa kike chuoni hapo hivyo amewataka wanafunzi hao wa kike kuongeza nguvu na kuwa wanafunzi bora wanaozingatia masomo yao hasa upande wa masomo ya Sayansi ili kusaidia kufanikisha lengo la Chuo katika kuiendeleza nchi kwa kuwa nchi haiwezi kuendelea kama haina nguvu kazi ya kutosha.
Prof. Chibunda amesema kuna vipaumbele vingi sana kwa watoto wa kike nyakati hizi hivyo jambo la msingi kwao ni kuwa wanafunzi wazuri wanaozingatia masomo yao pamoja na kizitumia fursa mbalimbali zilizopo zitakazowasaidia kufika kule wanakohitaji ikiwemo kutumia fursa ya udhamini wa wanafunzi katika elimu ya juu waliofanya vizuri masomo ya sayansi yaani MAMA SAMIA SCHOLARSHIP.
‘‘Dhumuni letu kama Chuo ni kuhakikisha tunafikia asilimia 50 ya wasichana katika Chuo chetu yaani tuwe na 50 kwa 50 kwa upande wa watoto wa kike na wa kiume hivyo tunawahamasisha watoto wa kike kusoma kwa bidii na tunaamini wana uwezo wa kufanya vizuri kwenye masomo yao hata kwenye masomo ya Sayansi ili kuiendeleza nchi yetu, hivyo tunawasihi kuwekeni na nguvu kwa kuwa kupitia juhudi zenu tutaweza kufikia lengo’’, amesema Prof. Chibunda
Kwa upande wake Bi. Paulina Lusisye ambaye ni Msimamizi Mkuu na Mwakilishi kutoka Shule ya Sekondari SEGA amesema kuwa kitu kilichowahamasisha kufanya Ziara katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ni kwamba wanaamini chuo hicho ni kikongwe na kizuri kwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kutokana na Mipango pamoja na Miradi ambayo inafanyika chuoni hapo ambayo ni Endelevu na inayowaweza kumsaidia kijana yeyote kuweza kufanikisha maisha yake kwa kujiajiri mwenyewe.
Aidha amesema Ziara hiyo itakuwa chachu ya mabadiliko kwa kubadilisha fikra za vijana kuweza kujitegemea wenyewe kwa kuzingatia kwamba ajira kwa sasa sio kipaumbele bali kujiajiri mwenyewe hivyo wanakishukuru Chuo cha SUA kwa kuwapatia fursa ya kutembelea maeneo yao na kujifunza kwa kuona ambapo kumeleta hari mpya kwa wanafunzi wao.
Naye Asteria Andrea mmoja wa wanafunzi katika Ziara kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana SEGA amesema kile walichojifunza kwa kusikia na kuona hasa katika mfumo wa uongozi Chuoni hapo ambao umewapa fursa wanawake vimemuhamasisha kuipenda SUA zaidi na atahakikisha anafanya vizuri kwenye masomo yake ili apate nafasi ya kusoma Chuoni hapo.
Nuru Kilui ambae pia ni mwanafunzi katika Ziara hiyo kutoka Ilala Sekondari iliyopo jijini Dar Es salaam amesema Mazingira ya Chuo cha SUA ni mazuri na yanamuwezesha mwanafunzi kusoma pia mafunzo yanayotolewa yanamuwezesha mwanafunzi kujiajiri mwenywe na kwakuwa anapendelea mambo ya upishi hapo baadae anatamani kusoma SUA mambo ya lishe ili aweze kuwa bora zaidi upande huo.
KATIKA VIDEO
0 Comments