SUAMEDIA

UWABIATA wakipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kuboresha tiba asili

 

Na Calvin Gwabara

Umoja wa watengeneza bidhaa za asili Tanzania (UWABIATA) umepongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia watafiti wake kwa namna wanavyo walea Waganga wa tiba asili nchini na kufanya tafiti zinazoleta tija katika utoaji wao wa huduma.

Mwenyekiti wa UWABIATA Bw. Rajabu Hamisi Mbambwa akizungumza katika mkutano wa wadau wa tiba asili

Shukrani hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa UWABIATA Bw. Rajabu Hamisi Mbambwa wakatia akiongea na SUAMEDIA mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa kwanza wa kisayansi wa tiba asili nchini uliofanyika SUA Mkoani Morogoro na kuwakutanisha Waganga wa tiba asili kutoka nchi nzima,watunga sera,Wizara ya Afya na watafiti kutoka taasisi mbalimbali za utafiti nchini zinazohusiana na tiba asili.

“Matabibu wengi wa tiba asili elimu yao sio kubwa na wengine hawakusoma kabisa lakini SUA wametutambua na kutupokea lakini kubwa zaidi wameithamini tiba asili na kwa muda sasa tunafanya kazi nao katika kufanya tafiti na kuboresha namna ya utengenezaji wetu wa dawa asili kutoka kienyeji na kutengeneza kisasa kufikia viwango na masoko ya ndani na nje” alisema Bw. Mbambwa.

“Aliongeza wakati tupo kwenye maonesho tumepata maelezo katika banda la SUA kutoka kwa mwananfunzi anayesoma Shahada ya Udaktari wa Falsafa katika maswala ya tiba asili, hakika hili limetupa faraja sana kuona wasomi wanaamua kubobea katika kuifanya tiba asili ifanye kazi kisasa badala ya kubaki na mbinu za jadi”.

Mwenyekiti huyo wa UWABIATA ameiomba SUA kuendeleza jitihada hizo za mashirikiano ili kuwawezesha watengeneza dawa za asili Tanzania kutengeenza bidhaa bora ambazo zitakidhi viwango vya kimataifa na hivyo kuwezesha dawa za Tanzania kuingia kwenye masoko ya dunia kama ambavyo dawa za nchi kama China na India zinavyouzwa kwa wingi nchini.

Umoja wa Watengenza Bidhaa za Asili Tanzania UWABIATA ni matokeo ya matunda ya kazi kubwa zilizofanywa na SUA kupitia Mradi wake wa GRILL na VaSPARD inayolenga kuongeza thamani za mazao yatokanayo na mimea dawa pamoja na kutumia teknolojia na ubunifu katika kuongeza kipato na kuboresha Maisha kupitia mimea dawa.

CG/GL                                 MWISHO.

Post a Comment

0 Comments