SUAMEDIA

SUA na Mradi wa Ubunifu (Innoversity Project) kutasaidia mawazo ya wanafunzi kuwa na Tija

NA GLADNESS MPHURU

Imeelezwa kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kushirikiana na Mradi wa Ubunifu (Innoversity Project) utasaidia wanafunzi kuhakikisha mawazo yao ya kibunifu yanakuwa na Tija wanapokuwa vyuoni na hata nje ya vyuo, kwa lengo la kupunguza ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Mradi huo Bi. Trufina Matekele Agosti 30, 2022 mkoani Morogoro, ikiwa ni siku ya pili ya Semina ya Mafunzo inayotolewa kwa Wanataaluma wa SUA ambayo itafanyika kwa siku tano 

"Mradi huu ni Mradi uliofadhiliwa na Ubalozi wa Ufaransa hapa Tanzania umelenga kuvijengea uwezo Vyuo vitatu ambavyo ni Wadau kikiwemo  Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Chuo Kikuu cha Iringa na Nelson Mandela African Institution of Science and Technology", amesema Meneja huyo.

Amesema mbali na Mafunzo hayo kwa Wanataaluma ambayo yamelenga kuwajengea uwezo kuwa tayari kuwasaidia Wanafunzi kwenye masuala ya bunifu, pia waliweza kuwakutanisha wanafunzi wa Vyuo hivi kuwaelezea dhumuni pamoja na fursa mbalimbali zitokanazo na mradi huo. 

"Tumefanikiwa kupata ushiriki mkubwa sana wa wanafunzi wakionesha nia ya wao kusaidiwa na kuhakikisha mawazo yao ya kibunifu yanakuwa na tija zaidi"

Ameongeza kuwa Chuo cha SUA ni Chuo cha Kilimo ambacho kinafursa nyingi ambazo ni masuala ya Kilimo na Ufugaji hivyo mradi huu unatoa nafasi kwa wanafunzi kuja na bunifu katika maeneo hayo ili waweze kusaidiwa.

Kwa upande wake Mratibu wa Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu Kutoka SUA Dkt. Doreen Ndossi, ambaye pia ni mshiriki katika mafunzo hayo, amesema kama Wanataaluma mafunzo hayo yatawawezesha kupata mbinu mbalimbali ya namna bora ya kulea bunifu na wabunifu.

" Tuko hapa kwaajili ya mafunzo mafupi ambayo sisi kama waalimu wa SUA tunapatiwa lakini hasa yanaendana na kituo chetu ama kitovu cha uvumbuzi tulichonacho pale SUA yaani SUA Innovation Hub", amesema Dkt. Ndossi.



Post a Comment

0 Comments