Na: Winfrida Nicolaus
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amewataka Chama cha Umoja wa Wakulima wa Umwagiliaji Msoga (UWAWAUM) kutoka Halmashauri ya
Chalinze Mkoani Pwani kushirikiana na SUA katika shughuli zao za kilimo pindi watakapo wahitaji lengo likiwa kuinua Kilimo nchini na kukifanya kuwa endelevu.
Prof. Chibunda ametoa wito huo wakati akizungumza na Wanachama hao walipofanya ziara katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa lengo la kujifunza na kujionea kwa macho shughuli mbalimbali za kilimo chuoni hapo hasa kilimo cha mbogamboga.
Amesema ni vyema kukifanya kilimo kuwa cha kisasa kwa kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo hasa katika matumizi ya Miundo Mbinu ya umwagiliaji na kuondokana na zana ya kutegemea mvua kwaajili ya kilimo.
"Naomba mkajipange kwa kitu chochote kile ambacho mmekiona SUA na kinaweza kuwasaidia hivyo mkiwa tayari na mtakapotuhitaji milango iko wazi lakini kikubwa zaidi muende mkawahamasishe vijana kujikita katika kilimo kwani kilimo kitawasaidia kujikwamua kimaisha vilevile kama mlivyoona tuna Kituo chetu cha ATAMIZI ambacho ni mahususi kwaajili ya kuwasaidia vijana waleteni vijana wenu waje wajifunze na waje kuwa chachu na msaada katika shughuli zenu za kilimo", amesema Prof. Chibunda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha UWAWAUM Bw. Joel Yohana Kipandwa amesema ziara yao ndani ya SUA ni yamafanikio makubwa kwani imewawezesha kujionea na kujifunza mambo mbalimbali katika kilimo hivyo kupitia ziara hiyo wataenda kuwa chachu na kuhakikisha wanaboresha kilimo katika eneo lao hasa kutumia mafunzo hayo katika Mradi wao wa Umwagiliaji ambao wanao kupitia kilimo cha mbogamboga wanachokifanya.
Bw. Gerald Francis Muyuwa Makamu Mwnyekiti wa UWAWAUM amesema uwepo wa Taasisi kama SUA nchini ni fursa kubwa kwa wakulima kama wao walivyoipata hivyo kupitia kile walichokiona na kujifunza chuoni hapo wanaahidi kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wakulima kutembelea SUA ili kujifunza hivyo kupitia mafunzo watakayoyapata yatawasaidia kukifanya kilimo chao cha Asili walichokizoea kuwa cha kisasa na chenye Tija.
Naye Bi. Rehema Hamisi Mtendaji wa Kijiji cha Msoga amesema kuwa Elimu haina mwisho hata mkulima anatakiwa ajifunze kila siku lengo likiwa ni kujikwamua kiuchumi na matamanio yao ni kuona wakulima wa Msoga wanalima kilimo chenye Tija na cha Kisasa kwaajili ya maendeleo hivyo SUA imekuwa sehemu sahihi ya wao kuja kujifunza na wamejionea kwa macho mambo mazuri na ya faida kwao kama wakulima.
KATIKA VIDEO







0 Comments