Na: Amina
Hezron, Mbeya.
Zaidi ya
Miche ya Miti 50,000 rafiki wa maji na vyanzo vya mito imeoteshwa na Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS) kwa
lengo la kurejesha uoto wa asili kwenye
vyanzo vya maji vya Mto Mbarali.
Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili akiangalia Miche alipotembelea Kitalu cha Miti Rafiki wa maji katika Kata ya Mdandu Wilayani Wanging’ombe Mkoani Njombe. |
Akizungumzia
miche hiyo Mtafiti na Mratibu wa Mradi wa EFLOWS kutoka SUA Dkt. Winfred Mbungu
amesema kuwa Vitalu hivyo vya miche vimepandwa katika Wilaya ya Mbarali mkoani
Mbeya na wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe ambazo Mto Mbarali unaanzia na
kuishia.
“Mto Mbarali
unaanzia mkoani Njombe ambako ndiko vyanzo vyake vilipo lakini unapita na
kuishia kwenye wilaya ya Mbarali na maji yake kuingia katika mto Ruaha Mkuu
ambapo tumeona kuanzia juu hadi chini kuna uharibifu mkubwa katika vyanzo vyake
na kandokando ya Mto kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu hivyo
kama mradi tumeona tusifanye utafiti pekee bali tushiriki pia kwenye kurejesha
uoto wa asili kwenye eneo lote”, alisema Dkt. Mbungu.
Mratibu
huyo wa Mradi amesema Mbegu za miche iliyooteshwa imechukuliwa kwenye miti
Rafiki ambayo imekutwa kwenye vyanzo hivyo na kandokando ya mto ambayo jamii
imeipendekeza na kuthibitisha ni miti rafiki kwa maji ili kuhakikisha miti yote
itakayopandwa iwe miti sahihi isiyoharibu vyanzo na kingo za mito.
Kwa
upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi huo Prof. Japhet Kashaigili amesema zoezi
hilo la upandaji wa miti pia wanashirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS)
kwa maana ya kusaidia utaalamu na usimamizi pamoja na Jumuiya za Watumia maji
Mbarali (JUWAMBA) ili kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja katika kutunza kitalu na
miche itakayopandwa ili zoezi liwe endelevu.
“Tunapanda
miti hii kama mbegu tu kwenye mawazo ya watu wote wanaoishi kandokando ya mto
huu na vyanzo vyake vya maji waone umuhimu wa utunzaji wa mito kwa maana ya kwamba
kama mazingira yatatunzwa vizuri kuanzia mto unapoanzia hadi unapoishia
utasababisha kuwe na maji yanayotiririka mwaka mzima lakini pia mto
utatiririsha maji ambayo ni salama kwa binadamu wanaoyatumia njiani pamoja na
Samaki na wadudu wengine waliomo ndani ya mto na wale walio baharini mto
unapoishia”, alifafanua Prof. Kashaigili.
Prof.
Kashaigili ameongeza kuwa kwa kufanya zoezi hilo kwa vitendo litawasaidia
wananchi wote kujua miti inayofaa kupanda kwenye vyanzo vya maji na mito lakini
pia kuwajengea uwezo wa kujua faida na umuhimu wa kupanda miti, pia wanatarajia
kupeleka miche ya miti ya matunda ambayo ni rafiki wa maji ili waweze kupanda
pia kwenye mita 60 za mito ili jamii iweze kujipatia kipato badala ya kupanda
miti tu pekee ambayo haiwasaidii katika uchumi wao.
“Wakati
huu ambao tunaelekea mwisho wa Mradi maana tumefika nusu ya muda wa utafiti
wetu tunaendelea kufikiria vitu
mbalimbali kutokana na Utafiti wetu ili tuache mahali ambapo jamii inaweza kuja
kujifunza kwa vitendo masuala ya Uhifadhi wa Mito na vyanzo vyake katika maeneo
mbalimbali nchini kuja kujifunza maana changamoto za uharibifu ni kilio
kilichopo maeneo mbalimbali ya mito nchini”alieleza Prof. Kashaigili.
Kwa
upande wake Mtafiti Msaidizi wa Mradi wa EFLOWS, Bw. Nyemo Chilagane amesema kuwa kitalu hicho
kilianza kuandaliwa mwezi wa nne mwaka huu kwa kushirikiana na JUWAMBA kwa
kuokota mbegu za miti aina ya Mizambarau na Mizambarau pori iliyo kandokando ya
mto na kisha kuiweka kwenye viriba na kuanza kuihudumia hadi sasa ambapo imefikia
hatua ya kupandwa.
Nae
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji (MBUMTILU) wilayani Wanging’ombe mkoani
Njombe Bw. Asheri Kilasi amewashukuru watafiti kutoka SUA kwa kuwezesha
kupatikana kwa kitalu hicho kizuri cha miche ya miti Rafiki wa maji kwa kuwa
wamekuwa wakihangaika katika kutengeneza vitalu bila mafanikio.
Amesema
kuwa katika eneo ambalo jumuiya yao inasimamia kuna vyanzo vya mito 176 ambavyo
vinachangia maji kwenye mto Mbarali lakini katika vyanzo hivyo vipo ambavyo
vina hali mbaya kutokana na kuharibiwa na vipo ambavyo bado vina hali nzuri
lakini jitihada zinahitajika katika kuvitunza.
“Kwa sasa
tumepata elimu Wanajumuiya wote tunajua mbinu za uoteshaji kitalu na miti
inayofaa kupandwa kwenye vyanzo vya maji na kando ya mito na tupo tayari kwa
zoezi la kwenda kuipanda maana imeshafikia hatua ya kupandwa ili tuotoshe miti
mingine tena lengo letu kubwa ni kuhakikisha Mto wetu na vyanzo vyake
vinafunikwa na miti rafiki na maji yanatiririka mwaka mzima maana tunahitaji
maji katika shughuli mbalimbali za kila siku kwenye Maisha yetu”, alieleza
Kilasi.
Kazi hiyo
inayofanywa na Mradi wa EFLOWS ni utelezaji wa Programu ya usimamizi endelevu
wa Madakio ya maji kupitia tathimini ya kuimarisha mtiririko wa maji kwa
mazingira na utekelezaji wake katika kulinda ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya
Hindi kutokana na athari za shughuli za kibinadamu (WIOSAP).
Hosea Kinyaga (kushoto) akimuonesha Mkuu wa mradi wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili (Kulia) Miche ya Zambarau kabla ya kupelekwa kwenye maeneo ya vyanzo ya maji kwa kupandwa. |
0 Comments