SUAMEDIA

SUA imetajwa kuwa ni fursa katika Sekta ya Kilimo kwa Mchango wa Maendeleo ya Taifa

Na: Gladness Mphuru

Mkuu wa Idara ya Uchumi Kilimo na Biashara kutoka Ndaki ya Uchumi na Biashara, Dkt. Fulgence Mishili akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda, kwenye Kongamano la Wadau wa Kilimo mkoani Morogoro


Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetajwa kuwa ni fursa katika Sekta ya Kilimo kwa mchango wa Maendeleo ya Taifa hususan mkoa wa Morogoro kutokana na kuwa msaada mkubwa kwenye kutatua changamoto za kilimo na ufugaji.

Hayo yamebainishwa Septemba 28, 2022 mkoani Morogoro, na Mkuu wa mkoa huo Fatma Mwasa, Mkuu wa wilaya ya Morogoro Albert Msando, Mkuu wa Idara ya Uchumi Kilimo na Biashara kutoka Ndaki ya Uchumi na Biashara, Dkt. Fulgence Mishili akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo cha  SUA Prof. Raphael Chibunda, pamoja na wadau wa Kilimo Morogoro, kwenye Kongamano la wadau wa kilimo mkoani humo lenye Lengo la kujadili Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na uhifadhi wa Mazingira.

Akizungumza katika Kongamano hilo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa amesema suala la mgogoro wa wakulima na wafugaji linatokana na ukosefu wa malisho kwa wafugaji hata kuvamia mashamba ya wakulima, hivyo amewaasa wakulima na wafugaji kukitumia Chuo cha SUA kupata elimu ili kufuga na kulima kwa tija bila kuharibu mazingira.

“Morogoro ni moja kati ya mikoa inayoongoza kwa shughuli za kilimo na ufugaji lakini tuna bahati sana kuwa na Chuo hiki cha Kilimo tutumie chuo hiki kama fursa kwetu ili kuzalisha kwa tija” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

Kwa upande wake Dkt. Mishili amesema kuwa Chuo cha SUA ni fursa katika Kilimo ,mafunzo na usambazaji wa Teknolojia za kisasa ikiwa ni pamoja na mbegu za kisasa za mazao mbalimbali hasa yanayopatikana mkoani Morogoro.

“Pamoja na teknolojia hizo, changamoto kubwa ni Teknolojia ya kupima udongo baadhi ya wadau wanasema kuwa wanaijua teknolojia ile lakini bado imekuwa ni ghari kwao kwa mtu mmoja mmoja kuifanya hivyo basi wameshauri Serikali iwapatie ruzuku katika kupima udongo maeneo ya vijiji lakini pia wadau wamehitaji kutoka kwetu SUA ni kuainisha maeneo ya kilimo na aina za mbegu zinazofaa katika eneo husika mfano zao fulani linafaa kulimwa eneo fulani labda Kilosa ama Mvomero”, amesema Dkt. Mishili 

Akizungumzia upande wa mazingira amesema inawezekana kuusaidia mkoa kwa njia ya mafunzo kwa kufundisha namna bora ya kufanya kilimo husika, kutengeneza programu za Ugani za kuweza kufikia na kuwapatia elimu wakulima kuhusiana na utunzaji wa Mazingira.

“Kwa hapo tunaweza kushirikiana sana na Serikali tena tunaweza kutumia Taasisi yetu ya ICE tukaweza kutengeneza masomo mbalimbali ya kuweza kuelimisha wakulima namna bora ya kufanya shughuli za utunzaji wa mazingira lakini tuweze kuwafikia wafugaji ili waweze kuwa wanapanda na kuzalisha malisho yao wenyewe ili kupunguza mtindo wa kuhamahama”, amesema Dkt. Mishili

Akizungumza kwa niaba ya wadau wa kilimo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Dkt. Christine Ishengoma ametoa wito kwa vijana kushiriki katika kilimo kupitia vituo Atamizi vilivyopo SUA, SUGECO na PASS.

Kongamano hilo limeongozwa na kauli mbiu isemayo “Kilimo ni Biashara hifadhi Mazingira”.


VIONGOZI MBALIMBALI WA MKOA WA MOROGORO WAKIONGOZWA NA MKUU WA MKOA HUO FATMA MWASA, MKUU WA WILAYA YA MOROGORO ALBERT MSANDO KWENYE KONGAMANO LA WADAU WA KILIMO MKOANI MOROGORO.















Post a Comment

0 Comments