Na: HADIJA ZAHORO
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Maktaba ya Taifa ya Kilimo iliyopo chuoni hapo kimeanzisha kitabu chenye jina la Kilimo cha Kisasa Mkononi Mwako (Mboga App), chenye lengo la kuwafundisha vijana mbinu mbalimbali za uzalishaji wa mbogamboga ili kujiajiri kupitia Sekta ya Kilimo.
Akizungumza kupitia kipindi cha Kapu la Leo kinachorushwa na SUA FM, Afisa Maktaba Bw. Shabani Omary Chika amesema kitabu hicho ni moja kati ya hazina walizoaamua kuonesha kwa vijana ambazo zinaweza kuwa muarobaini wa vyanzo vidogovidogo vya mapato.
Ameeleza kuwa ndani ya hazina hiyo kuna maarifa yaliyojificha yanayoweza yakamfumbua macho kijana na kumtoa kutoka hatua moja kwenda nyingine
Aidha, Bw. Chika amesema kuwa vijana wamekuwa wakilalamika kuhusu ugumu wa maisha lakini kupitia kitabu hicho anaweza kujifunza jinsi ya kuotesha mbogamboga akiwa nyumbani hata kama ni katika eneo finyu.
Amesema licha ya kitabu hicho kuwa na nakala ngumu pia kinapatikana katika simu janja kwa kuipakua ambayo imeeleza mbinu zote za upandaji wa mbogamboga ikiwemo namna ya kulima, kuandaa kitalu, mazingira ya kuandaa kitalu, namna ya kumwagilia pamoja na namna ya kuotesha mbegu.
‘‘Hichi kitabu pamoja na kuwa tu kipo kwa nakala ngumu lakini pia kuna aplikesheni ambayo vijana wengi wamekuwa na simu janja angeweza tu kuingia katika simu janja yake akaenda kwenye "play store" akaandika tu Mboga App, akakutana na app hii na ikampa mazingira yote namna ambavyo anaweza kulima, namna anaweza akaandaa kitalu namna ya kuotesha kitalu na vitu vyote vimeelezwa katika app hii’’. Anaeleza Bw. Chika
Kwa upande wake Bi. Editha Njeu ambaye pia ni Afisa wa Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo, ameeleza kuwa kitabu hicho kimeonesha mambo mbalimbali ikiwemo kujua uchaguzi wa eneo lenye uwezo kumudu upatikani wa mbolea, maji pamoja na wateja ili kuepuka gharama.
Amesema kitabu hicho kilichoandikwa na Mkufunzi kutoka chuoni hapo Teophilda J. Maginga kimeelekeza pia sio lazima kununua madawa ya madukani badala yake unaweza ukatumia dawa za asili kama vile kupanda miti au majani mbalimbali yanayoweza kufukuza wadudu ili kuepuka kuingia gharama kwa vijana wasio na mtaji.
0 Comments