Na Editha Mloli
Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameendelea kufanya juhudi za kutatua changamoto za uhaba wa malisho, uharibifu wa mazingira na ukosefu wa ajira kwa wanawake na vijana na wameanza utekelezaji wa mradi wa Tekinolojia ya Juncao kwa kuanza kuzalisha na kusambaza mbegu za nyasi aina Juncao Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.
Teknolojia hii inahusisha
matumizi ya nyasi aina ya JUNCAO katika uzalishaji wa uyoga, kuhifadhi ardhi,
kuzuia mmomonyoko wa udongo, pamoja na malisho kwa ajili ya mifugo ambapo asili
yake ni kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu (FAFU) kilichoko Jimboni Fujian,
nchini China.
Akizungumza na SUA MEDIA Mtaalamu
wa teknolojia ya JUNCAO kutoka Idara ya Sayansi za Elimu ya Viumbehai
(Biosciences), Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi ya SUA, Dkt. Elly Ligate,
amesema kwa kushirikiana na watafiti na maafisa kilimo visiwani Zanzibar
wameanzisha vitalu vya nyasi hizo katika mashamba ya majaribio yaliyoko katika
kituo cha utafiti wa mifugo kilichopo Kizimbani Unguja na Chamanangwe kisiwani
Pemba.
Ameendelea kwa kusema kuwa kwa upande wa Tanzania bara wataalamu kutoka SUA wameshirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanya majaribio ya uzalishaji wa nyasi hizo katika wilaya zipatazo 11 kwenye mikoa tofauti na Mbegu za Nyasi za Juncao zimeshasambazwa kwa wakulima katika wilaya za Geita, Kilindi, Handeni, Kibaha, Kigamboni, Bumbuli, Chalinze, Kilosa, Bahi, Mbarali, Dodoma pamoja na Ubungo na Kinondoni.
Dkt. Ligate amefafanua
kwamba vituo hivi vitatumika katika
kuzalisha mbegu za kutosha ili ziweze kusambazwa kwa wakulima na wafugaji
nchini Tanzania ambapo Matarajio yao makubwa ni kuwafikia wafugaji wengi katika
visiwa vya Zanzibar na Bara kwa kuwa mahitaji ya malisho ni makubwa katika
kuelekea kuimarisha sekta ya mifugo nchini.
“Juhudi za kutekeleza Tekinolojia ya Juncao nchini
zilianza mwanzoni mwa mwaka 2021 na
zimeendelea kuenea nchi nzima na Kila tuliko peleka mbegu wakulima wameonesha
kuzikubali” anasema Dkt. Ligate
Ingawa wameanza na uzalishaji wa malisho,mtaalamu na
mratibu wa wa Teknolojia ya
JUNCAO nchini Tanzania, Dkt Ligate ametoa wito kwa Watanzania kuwa tayari
kuipokea na kuitekeleza tekinolojia hii kwa mapana yake ili kwamba Pamoja na
uzalishaji wa malisho, lakini pia watazalisha Uyoga ili kujipatia kipato na
kuhifadhi mazingira nchini Tanzania.
Wafugaji walioanza kuzalisha
nyasi za Juncao, wamenufaika kwa kiasi kikubwa na wamekuwa na matokeo chanya
ambapo wiki iliyopita Dkt Elly Ligate na Maafisa kutoka Wizara ya Mifugio na
Uvuvi walitembelea mashamba yaliyoko Dodoma kujionea maendeleo ya nyasi za
Juncao pia mashamba ya mfano kule visiwaniVisiwani Zanzibar na ili kuona jinsi
hali inavyoendelea.
Dkt. Ligate ametoa shukrani kwa
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Fujiani cha Kilimo na
Misitu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tanzania bara, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji,
Maliasili na Mifugo ya Zanzibar, pamoja na wadau binafsi kama vile Ndugu Albert
Marwa kwa kufanikisha kuenea kwa tekinolojia ya Juncao nchini Tanzania.
0 Comments