Na Amina Hezron,Mbeya
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia ufadhili wa Taasisi inayojishughulisha na tafiti za utunzaji wa Bahari (WIOMSA) wameendesha mafunzo ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo Wanasayansi, Mameneja na wadau wengine namna ya kuendesha na kufanya tathimini ya Maji kwa Mazingira katika ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Akifungua mafunzo hayo Septemba 19, 2022 Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Reuben Mfune amewataka wadau waliopata mafunzo hayo kuhakikisha wanakwenda kuyafanyia kazi na kuwafundisha wengine kwenye ofisi wanazotoka ili kutimiza malengo ya mafunzo.
“Wale ambao wako ukanda wa juu ya mto
unakoanzia wanatakiwa kujua fika shughuli za uharibifu wanazozifanya kule ndizo
zinazoleta athari kwenye mabwawa ambayo yanajaa tope ambalo linakwenda mpaka
Baharini na kuaathiri viumbe vilivyomo katika Mito, Maziwa na Bahari”, alisema
Mhe. Mfune.
Mhe Mfune amewapongeza SUA na
WIOMSA kwa kuandaa mafunzo hayo kwa kuwa yanaendana na kazi inayoendelea ya
kurejesha afya ya Mito na kupunguza madhara yanayotokana na uchafuzi wa
Mazingira katika mito, kwani ni jambo jema kufanyika na litakuwa msaada mkubwa
kwa Taifa.
Aidha amewataka wadau wengine
kuendelea kujitokeza kusadia jitihada za Serikali na wadau waliopo sasa ili
kuhakikisha Mito inaendelea kutiririka mwaka mzima na hivyo kuwataka Wananchi
kuheshimu Sheria zilizowekwa kwakuwa zipo kwa manufaa ya Watanzania wote.
Akizungumzia mafunzo hayo Mtafiti
Mkuu wa Mradi huo kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema lengo kubwa la
mafunzo hayo ni kujenga Wataalamu na utaalamu wa kuweza kufanya tathimini ya
maji kwa mazingira ili kusaidia wanapofanya maamuzi katika kugawana maji iwe
kwa ajili ya maendeleo endelevu.
“Ni mafunzo ya kujenga uwezo
ambayo yana vitendo ndani yake. Wataona shughuLi zinazofanyika kama sehemu ya
kuhifadhi mazingira na kilichopelekea shughuLi hizo zifanyike pamoja na sababu
za msingi za kuwezesha kwanini hiyo tathimini ya maji kwa mazingira ifanyike na
shughuli gani zifanyike kwenye maeneo hayo. Hivyo mahari kwingine watafanya wao
wenyewe kama sehemu ya mazoezi”, alisema Prof. Kashaigili.
Prof. Kashaigili amefafanua kuwa
tathimini hiyo ya maji kwa mazingira itawezesha kuhusanisha madhara
yanayotokana na shughuli mbalimbali zinazozifanywa na kwa kiasi gani
zinapelekea kuathiri Ukanda wote wa
Bahari ili kuweza kujua chanzo cha
tatizo, hatua tatizo lilipofikia,
madhara na namna ya kutatua.
“Hii itasaidia nchi kutekeleza
Sera ya Maji pamoja na Sheria ya maji ya mwaka 2009 ambayo imeainisha katika
kugawana maji kwa vipaumbele ni kwa ajili ya matumizi ya Binadamu, Mazingira na
kwa shughuli nyingine, hivyo maji kwaajili ya mazingira ilikuwa ni sehemu
ambayo haina utaalamu na hakukuwa na jinsi ya kufanya hivyo bila kujenga
utaalamu sasa utaalamu upo hivyo ni lazima tujenge sasa Wataalamu wengi “,
alisema Prof. Kashaigili.
Kwa upande wake Meneja wa
Programu ya Mazingira ya Bahari (WIOMSA) ambao ndio wafadhili wa mafunzo hayo,
Dkt Mathias Igulu amesema kuwa kuna mahusiano makubwa kati ya Bahari na Mito,
lakini jambo hilo halijaongelewa sana ndio maana WIOMSA wameona ni vyema
kuanzisha mjadala na kuwaleta pamoja Wanasayansi na wadau wengine kwa maslahi mapana ya uhifadhi wa Bahari,
Mito na Mazingira.
“Kwa kushirikiana na Chuo chetu
kikubwa cha SUA ambacho wote tunajua wana Wataalamu wabobevu kwenye maswala ya
Sayansi za Kilimo, Maji na Mazingira, Ufugaji wa Samaki na Sayansi zingine
zinazoendana na hizo tumeona ni muda muafaka kushirikiana nao kuwaleta pamoja
wadau muhimu nchini na nje ya Tanzania kwa kuwa wanao uwezo mkubwa wa kusimamia”Alisema
Dkt. Igulu.
Akizungumza mmoja ya washiriki wa
mafunzo hayo, Mtafiti Msaidizi kutoka Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi (TAFIRI) Bi.
Wendo Lukwambe amesema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwao kwakuwa
yatawasaidia kujua jinsi mtiririko wa maji unavyoenda na namna ya kutunza maji
kwa mazingira kwakuwa isipofanyika hivyo itasababisha kuathirika kwa maji hayo.
Mafunzo hayo ya siku tano
yamewahusisha washiriki kutoka Taasisi mbalimbali za Utafiti katika sekta za
Maji, Mazingira, Misitu na washiriki
wengine kutoka nchi za ukanda wa magharibi mwa Bahari ya Hindi ikiwemo Afrika Kusini, Kenya, Mauritius, Msumbiji,
Visiwa vya Shelisheli, Somalia, , Visiwa vya
Comoro, Madagasca na Visiwa vya Reunion ambao wameshiriki kwa njia ya
Mtandao (Zoom).
Meneja wa Programu ya Mazingira ya Bahari (WIOMSA) ambao ndio wafadhili wa mafunzo hayo, Dkt Mathias Igulu akitoa salamu za Taasisi yao umuhimu wa mafunzo hayo kwa nchi wanachama. |
0 Comments