Na: Gojo Mohamed
Katika
kuhakikisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa unadhibitiwa nchini Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) kupitia Hospitali yake ya Rufaa ya Wanyama kwa kushirikiana na
Manispaa ya Morogoro kimeweza kutoa elimu, ushauri pamoja na chanjo kuhusiana
na ugonjwa huo katika Kata ya Bigwa na Mindu zilizopo Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza katika zoezi hilo Septemba 28 mwaka huu, Daktari Mkuu wa Hospitali hiyo Isack Kashoma amesema ugonjwa wa kichaa cha mbwa unasababishwa na kimelea cha Kirusi na ni ugonjwa ambao unawapata Wanyama wafugwao kama vile mbwa, paka ng’ombe, mbuzi na hata Wanyama pori kama vile fisi waking’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huo.
“Na sisi kama Hospitali ya Rufaa
ya Wanyama tulipewa Kata mbili ambazo ni Mindu na Bigwa, katika kata ya Mindu
tulikuwa na vituo vinne ambavyo ni Lugala,
Kasanga, Mindu sekondari pamoja na Madaganya na katika Kata ya Bigwa
tulikuwa na vituo vinne ambavyo viliweza kutoa huduma hiyo na mwitikio ulikuwa
ni nzuri”, amesema Dkt. Kashoma.
“Na katika
Kata ya Mindu tumeweza kuchanja Wanyama si chini ya 140 huku Kata ya Bigwa wakichanja
zaidi ya mbwa 200 na hili zoezi litaendelea hadi tarehe 2 mwezi wa 10 mwaka huu
hadi pale kampeni ya kitaifa itakapo malizika”, amesema
Dkt.huyo.
Ameongeza
kuwa anawakaribisha wafugaji ili waweze kupeleka mbwa wao katika Hospitali ya Rufaa
ya Wanyama iliyopo SUA ili kuweza kupatiwa chajo ambayo inatolewa bure katika
kipindi chote cha kampeni hii ya kitaifa na kusisitiza kuwa chanjo hii muhimu
kwa sababu mbwa akishapata ugonjwa huu hawezi kupona.
Amesema
binadamu anaweza kupata ugonjwa huu kupitia kung’atwa na mbwa mwenye kichaa au
kugusa majimaji hasa mate ya mbwa mwenye ugonjwa huo.
Kwa upande
wa Bi. Resti Longo na Bw. Kedimundi Ngewe
ambao ni wakazi wa Lugala wamekishukuru Chuo cha SUA kwa kutoa chanjo
hiyo na kuwahamasisha wafugaji kujitokeza ili mbwa wao waweze kuchanjwa.
Zoezi hilo
la utoaji wa chanjo ya kichaa cha mbwa limejumuisha baadhi ya Wanafunzi wanaosoma
Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Tiba ya Wanyama na Mifugo kutoka SUA kwa lengo
la kuwajengea uwezo na uzoefu katika masomo.
![]() |
Mwanafunzi
wa Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Tiba ya Wanyama na Mifugo akishiriki kutoa Chanjo
ya Kichaa cha Mbwa ili kuweza kuongeza ujuzi katika ikiwa ni Kampeni ya kitaifa. |
![]() |
| Mfugaji wa Mbwa akiwa anasubiria Mbwa wake waweze kupatiwa Chanjo ya Kuthibiti Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa katika Mtaa wa Lugala Kata ya Mindu Manispaa ya Morogoro. (Picha na Gojo Mohamed) |
![]() |
| Paka aliyeletwa na kupatiwa Chanjo ya kuzuia Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa katika Mtaa wa Madaganya Manispaa Ya Morogoro. (Picha na Gojo Mohamed) |
![]() |
| Dkt. Isack Kashoma akiwa na Bi. Resti Longo ambaye alimpeleka Mbwa wake kupatiae Chanjo ya Kichaa cha Mbwa katika Mtaa wa Lugala Manispaaa ya Morogoro. (Picha na Gojo Mohamed) |
![]() |
Dkt.
Isack Kashoma (aliyevaa Kofia) katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Udaktari wa Wanyama na Mifugo baada ya zoezi la kutoa chanjo ya Kichaa cha Mbwa Manispaa ya Morogoro.
|
|






0 Comments