SUAMEDIA

Malezi kuchangia Uboreshaji au kusababisha matatizo ya ugonjwa Afya ya Akili ya Mtoto

Na Editha Mloli

Suala la malezi kwa watoto limeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uboreshaji wa afya ya akili ya mtoto au kusababisha matatizo ya ugonjwa wa akili na kupelekea matukio mengi ya kikatili kushamiri ikiwemo kujiua au kufanya mauaji. 


Akizungumza na SUAMEDIA kuhusiana na afya ya akili Dkt. Pearson Mwemezi kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) amesema kuwa wazazi au walezi wamekuwa wanatengeneza kizazi chenye matatizo ya afya ya akili kwa kufanya vitendo vya unyanyapaa, kuwasema vibaya na matendo ya kikatili kama vile vipigo, na unyanyaswaji kingono.  

Amesema afya ya akili ni kutokuwa na ugonjwa au matatizo yoyote katika uwezo wa akili au fikra na kuweza kufanya jambo lililo sahihi na kupambanua mambo kwa wakati sahihi na kuyatolea maamuzi yaliyo sahihi.

Dkt. Mwemezi amefafanua kuwa Magonjwa ya Akili ni matatizo ya Ubongo ambayo yanampelekea mtu kutokuwa sawa kifikra, kihisia na kupelekea kushindwa kupambanua mambo na kufanya matendo tofauti katika jamii yake inayomzunguka.

Amesema hata kwa mtoto mdogo afya ya akili inazingatiwa kwa kuangalia umri pamoja na vitendo anavyovifanya kama vinaendana na umri wake na kama atakuwa akifanya vitendo ambavyo haviendani na umri wake inatathminiwa kuwa hapo mtoto atakuwa na matatizo ya afya ya akili.

Dkt. Mwemezi ameongeza kuwa kwa watu wazima matatizo ya afya ya akili kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na msongo wa mawazo ambapo mtu anashindwa kushirikisha watu hivyo kupelekea kuchukua hatua ikiwemo kuutoa uhai wake au wa mtu mwingine ambapo mpaka kufikia hatua hiyo ni mchakato na halitokei kwa mara moja.

“Unaweza ukakuta mtu kafukuzwa kazi ambayo ndiyo ilikuwa kila kitu kwa familia yake lakini mtu mwingine unaweza kuona kawaida lakini jambo hilo likampa msongo wa mawazo kiasi kwamba akaona hana faida ya kuendelea kuwepo tena duniani na kuchukua maamuzi magumu hata ya kujiua”.



Post a Comment

0 Comments