Na Amina Hezron,Morogoro
Katika kuhakikisha Afya ya Mlaji
na Mkulima inalindwa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Idara ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani
imetoa mafunzo kwa wakulima kuhusiana na matumizi ya mbinu za Kilimo Ikolojia
katika uzalishaji ambazo zitawasaidi kuepukana na matumizi ya pembejeo za
viwandani kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza katika Mafunzo hayo Mhadhiri kutoka SUA Dkt. Ramadhani Majubwa amesema kuwa kilimo ikolojia
kinalenga hasa kuhakikisha mkulima anatumia mbinu rafiki ambazo zinatunza
mazingira pamoja na kutunza viumbe hai ambao wanapatikana katika eneo husika.
“Tumelenga kuwafundisha wakulima
kuzalisha mazao ambayo hayatakuwa na sumu pamoja na kuwapunguzia athari
zinazoweza kutokea kutokana na upuliziaji wa dawa shambani ambazo mara nyingi
dawa hizo huweza kuwarudia wenyewe na kuweza kusababisha athari za kiafya”,
alisema Dkt. Majubwa.
Aidha amewataka wakulima
kuacha kilimo cha mazoea na badala
yake kuingia katika kilimo cha
kiikolojia kwa kuwa njia hiyo itawasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya
nchi yanaendelea kutokea duniani lakini pia kupunguza gharama za matumizi ya pesa
kwa ajili manunuzi ya pembejeo huku ikiongeza uzalisahaji wa mazao kutokana na
ongezeko la wadudu rafiki kama vile nyuki ambao wanasaidia katika
uchavushaji.
Kwa upande wake Mkulima kutoka katika Kijiji cha Ruvuma Kata ya Mlimani mkoani Morogoro Bi Chagua Kibwana ameipongeza SUA kwa mafunzo hayo na amewataka wakulima wengine kulima kilimo hicho ili kuepukana na gharama zisizo na msingi za ununuaji wa mbolea na badala yake utatumia mbolea za asili.
“Hapa nimeona mazao yaliyotumia
mbolea za asili yamenoga ukilinganisha na yale ambayo hayajatumia kabisa pamoja
na yale yaliyotumia pembejeo za viwandani kwa kweli nilikuwa sijui kama kuna
umuhimu wa kuwa na boksi la usafi shambani wala kama kuna wadudu rafiki
shambani, alisema Bi. Kibwana.
Naye Mkulima mwingine Bw. Geukeni
Asifiwe amesema kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kufahamu faida za kilimo hai
ambacho mojawapo ya mambo muhimu ni kutunza wadudu rafiki ambao husaidia kuua
wadudu shambani badala ya kutumia viuatilifu ambayo vinaathari hadi kwa walaji.
Mafunzo hayo ya siku tatu
yameanza na wakulima wa Kijiji cha
Ruvuma Kata ya Mlimani na Sept 13
watashiriki wakulima wa Kinyenze Vitonga na Mlali kabla ya wakulima wa Kiroka kutoka Morogoro
Vijijini.
0 Comments