Na:Hadija Zahoro
Katika kuhakikisha Mifugo inapata thamani ya lishe, Idara ya Mashamba ya Mafunzo ya Mfano iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA eneo la Magadu imeendelea na jitihada za kupukucha Mtama pamoja na kuuchakata kwa ajili ya Mifugo kwa kutumia mashine maalumu kwa lengo la kurahisisha kazi hiyo.
Farid Juma Chamkwata kutoka Idara hiyo katika Kitengo cha Shamba la Wanyama, amesema zoezi hilo ni endelevu kwa sababu Chuo kina mtama mwingi pamoja na vyakula vingine ambapo wamelima mashamba takribani heka 70 za mtama, 40 za mahindi na 60 za alizeti katika Mashamba ya Chuo kwa lengo pekee la kulishia mifugo.
Ameeleza kuwa mashine wanayotumia katika kupukuchia inarahisisha zoezi hilo kwa sababu unapotoka kuvuna mtama unakuwa na majani yake hivyo wanachakata zao hilo ili kuweza kupata nafaka safi kabla ya kuelekea kwenye hatua ya uchakataji wa chakula ili ng’ombe aweze kula.
“Mashine hii inarahisisha kwenye uchakataji kwa sababu unapotoka kuvuna mtama unakuwa katika majani yake kama unavyoona lakini baada ya hapo tunapiga ili kupata nafaka safi kwa ajili ya kwenda kwende uchataji wa chakula”, amesema Chamkwata.
Bw. Chamkwata ameongeza kuwa zao hilo la mtama lina virutubisho vingi vitakavyowezesha thamani bora ya lishe kwa mifugo, ikiwemo chanzo cha nguvu, protini, pamoja na mafuta kwa kiwango kidogo.
Aidha amesema kuwa wana mahindi na mashudu ambapo vyote wanavitumia kulisha wanyama waliopo shambani kwao ambapo kwa sasa wametumia takribani magunia 60 ambayo tayari wameshalishia wanyama kuanzia mwezi wa saba na mpaka sasa wana magunia 130 lengo likiwa ni kupata magunia 280 mpaka 300 kutokana na mtama ambao bado upo katika ghala lao.
Kwa upande wake Khatib Mohamed Luvanda kutoka Kitengo cha Malisho ambaye ndiye Mchakataji wa nafaka amesema zoezi la uchakataji linaongeza thamani na kurahisisha ulaji wa ng’ombe hasa wa maziwa na wasio wa maziwa kulingana na uhitaji wa afya ya mifugo.
Ameeleza kuwa mtama uliovunwa unachakatwa kutoka hali ya nafaka na kuwa katika hali ya unga na hatimaye kuchanganywa na vyakula vya kuchanganyia ikiwemo majani makavu yaliyosagwa katika mashine ya kuchanganyia kwa kutumia kanuni maalum kulingana na aina ya mfugo kama vile ndama na mifugo yenye mimba.
0 Comments