Uwepo wa Mabadiliko ya Tabianchi yatokanayo na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo uchomaji mkaa na kilimo kisicho zingatia hifadhi ya mazingira umeendelea kuathiri upatikanaji wa Rasilimali maji na kuilazimu Serikali kutumia fedha nyingi kurudisha Uoto wa asili na kuimarisha vyanzo vya maji nchini.
Kutokana na changamoto hiyo Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Global Water Patnership imepokea msaada wa sh. Milioni 460 kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC ili kuanza utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Rasilimali maji katika kustahimili Mabadiliko ya Tabianchi katika bonde la Wami Ruvu katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu.
Akieleza Manufaa ya Mradi huo Crisongonous Kibugu ambaye ni Afisa wa Mradi huo amesema Mradi utaimarisha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi lakini pia katika suala la kulinda na kuhifadhi mazingira kando ya vyanzo vya maji.
Aidha amesema Mradi huo umekuja kutokana na uwepo wa athari za mabadiliko ya tabianchi hasa kwenye vyanzo vya maji vinavyolindwa na Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu.
Kwa upande wake Dkt.Victoria Kongo MKurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo la Global Water Patnership amesema mradi huo unatarajia kuanzisha miradi mingine ya maji ikiwemo uchimbaji wa visima kwenye maeneo ambayo huduma ya maji imekuwa ikisuasua.
Pia amesema sasa ni muda kwa Wataalamu kutoka Sekta mtambuka zinazotumia rasilimaji maji kuleta mapendekezo ambayo yatamsaidia mkandarasi mshauri kuweza kutekeleza mradi huo kwa ufasaha pamoja na kubainisha changamoto zilipo katika maeneo ya vyanzo vya maji.
Naye Diana Kimbute ambaye ni Mhandisi wa Maji Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu amesema wao kama Wasimamizi wakuu wa vyanzo vya maji wako tayari kuhakikisha mradi huo unafikia malengo.
“Sisi kama Wasimamizi wakuu wa vyanzo vya maji Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu tutahakikisha mradi huu unafanikiwa na tutatoa ushirikiano wa kutosha, hii Miradi ni ya kwetu sote hizi athari za mabadiliko ya tabia nchi tuliona mwaka uliopita zilivyoleta shida na kusababisha Rasilimali maji kupungua kwa kiasi kikubwa na mkoa uliopata shida zaidi ni mkoa wa Dar salaam”, alisema Kimbute.
0 Comments