Winfrida Nicolaus
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
SUA kimeahidi kutoa kiasi cha sh. 1,000,000/= kila Mwaka kwaajili ya kukiunga
mkono Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA)
katika harakati wanazozifanya kwaajili ya kuboresha Elimu ya Hisabati
nchini ikiwemo utoaji wa Mafunzo kwa Walimu wa Hisabati.
Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu
wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akimwakilisha Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika
ufunguzi wa Warsha ya 56 ya Kitaifa ya Hisabati Tanzania na Mkutano Mkuu wa
Chama uliofanyika Kampasi ya Solomoni Mahlangu SUA.
Amesema CHAHITA kinahitaji
angalau Sekta ya Umma ili kukipa nguvu katika kushawishi Walimu wa Soma la
Hisabati kuhudhuria Warsha mbalimbali zinazotoa mafunzo katika kuboresha mbinu
za ufundishaji na ujifunzaji hivyo atashirikiana bega kwa bega na Uongozi wa
Chama hicho ili kuona wanachoweza kufanya katika kuishawishi Wizara ya Elimu
lakini kuishawishi Tamisemi katika kusaidia chama hicho kwenye shughuli zake.
Prof. Chibunda amesema Uongozi wa
Chama unafanya kazi kubwa sana katika kutatua hali mbaya ya ufaulu kwenye somo
la Hisabati lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya ikiwemo kujenga uelewa kwa
jamii kuhusiana na somo hilo.
“Wanahesabu hawa ni wa muhimu
sana lakini ujuzi wa hesabu walionao hauwapi wadau kama walivyo Wahandisi na
Wakandarasi kuwashawishi kwamba hii kampuni bila Hesabu isingesimama inaweza
kutuchukua muda kwa hiyo tutahitaji intervation ya angalau Sekta ya kiserikali
kuweza kusaidia hasa pande za pembezoni ambapo kuna shida kubwa katika soma
hili la hesabu hivyo tunahitaji nguvu ili walimu wa Hesabu kutoka maeneo yote
ya Tanzania kuhudhuria Warsha kama hizi” , amesemaProf. Chibunda
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Chama cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA) Bi. Betinasia Manyama amesema
changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na ufaulu hafifu wa somo la hisabati
hasa kwa ngazi ya Msingi na Sekondari ambapo kunachangiwa hasa na upungufu wa walimu kwa ngazi zote za
Elimu ambapo wameelemewa na idadi kubwa ya vipindi.
Changamoto nyingine ni
ukosefu wa Fedha za kuendeshea kazi
mbalimbali ndani ya chama ikiwemo nauli kwaajili ya kuwapatia waalimu kwenda
kufundishia mwezi wa tatu kila mwaka pamoja
na Walimu wa Hisabati kukosa Hamasa kutokana na kazi nyingi huku Mshahara ukiwa
ni uleule kwa walimu wote bila kujali mwalimu wa somo hili ana vipindi vingi na
somo lake linahitaji ufuatiliaji wa hali ya juu.
“Wastani wa waliofaulu katika
miaka tisa iliyopita katika mtihani wa Hisabati wa kitaifa kwa shule za msingi
ni asilimia 31.86 na katika shule za sekondari ni asilimia 76.46, kwa mfano
ufaulu wa Hisabati kwa kidato cha nne mwaka 2021 ni 19.54% hivyo ni vyema
Serikali kulipa somo la Hisabati umuhimu maalum maana ndio nguzo ya masomo yote
hasa masomo ya Sayansi na pia bila Hisabati hakuna Wahandisi na hivyo hakuna
Viwanda”, amesema Bi. Betinasia Manyama


0 Comments