Winfrida Nicolaus
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kushirikiana na
Wizara ya Afya kimeahidi kufanya kazi bega kwa bega na wadau mbalimbali waliopo
katika Mnyororo wa Thamani wa bidhaa za Tiba Asili kwaajili ya kuibua Bunifu na
kupata suluhisho la Kisayansi kuhusu changamoto zilizopo kwenye Mnyororo wa
Thamani wa Biashara ya Bidhaa za Mimea Dawa nchini.
Hayo yamebainishwa na
Mkurugenzi wa Uzamili, Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia kutoka Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Esron Karimuribo Agosti 29, 2022 wakati
akimwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam
Prof. Maulid Mwatawala ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye Kongamano la Kwanza la
Kisayansi la Tiba Asili Tanzania linalofanyika SUA Kampasi Kuu ya Edward
Moringe Sokoine.
Amesema uwepo wa Kongamano hilo la Kisayansi kuhusu Tiba Asili
ya Mwafrika lililowakutanisha Wadau mbalimbali waliopo katika Mnyororo wa
Thamani wa Bidhaa za Tiba Asili wakiwemo Wakulima wazalishaji, Wavunaji,
Watengenezaji, Wauzaji wa jumla na rejareja , Taasisi zinazosimamia Ubora,
Watunga Sera na Watafiti upo kwenye moja ya majukumu na malengo ya uanzishwaji
wa SUA.
Prof. Karimuribo amesema wanaamini lengo la Kongamano hilo ni
kuibua Bunifu na kupata suluhisho la Kisayansi kuhusu changamoto zilizopo kwenye
mnyororo wa thamani wa biashara ya Bidhaa
za Mimea Dawa nchini ili bidhaa hiyo iwe endelevu na iweze kutoa mchango
mkubwa kwenye kipato cha Wananchi kwa ujumla.
” Tunathamini sana mchango wa Sekta hii na tunaamini
tukishirikiana kwa pamoja tutafika mbali hivyo nasisitiza katika suala la
Ubunifu ili kuweza kuwa na Dawa Asili katika mfumo ambao unaweza kuupeleka
kwenye Pharmacy ili tuweze kujua kilichopo ndani, dozi ni kiasi gani hata hivyo
watafiti wameamua kujiongeza na kufanya Dawa hizi za Asili kuwa katika muundo
wa kama dawa nyingine tunazotumia”, amesema Prof. Karimuribo
Aidha Prof. Karimuribo amewahakikishia wadau wa Kongamano hilo
la Kwanza la Kisayansi la Tiba Asili Tanzania kuwa SUA kwa kushirikiana na
Serikali ya Tanzania itakuwa bega kwa bega nao katika kuhakikisha kuwa
yatokanayo na Kongamanola hilo yanapewa kipaumbele katika kazi zao za Utafiti,
Mafunzo na kuwa endelevu ili kuboresha Bidhaa hizo za Tiba Asili.
Kwa upande wake Dkt. Paul Mhame kutoka Wizara ya Afya
amekiomba Chuo cha SUA kuwasaidia kufanya Utafiti wa namna ya kulima na kupanda
Miti Dawa katika kiwango kinachokubalika.
0 Comments