Editha Mloli
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimeahidi kuendelea kushirikiana
na Wizara ya Afya katika mambo mbalimbali ambayo yanashabihiana na Mrengo wa
Chuo katika kuisaidia jamii hasa wale wanaohusika na masuala ya Tiba Asili na
Tiba Mbadala na kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa katika Kongamano la
Kwanza la Tiba Asili ya Mwafrika hapa nchini.
Hayo yamezungumzwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Sokoine Cha Kilimo SUA Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid
Mwatawala wakati akifunga Kongamano la Kwanza la Tiba Asili ya Mwafrika
lililofanyika Mjini Morogoro katika Chuo cha SUA.
Prof. Mwatawala amesema Chuo kitazibeba changamoto pamoja na
mapendekezo yaliyotolewa na Wadau wa Tiba Asili na Tiba Mbadala na kuona namna gani kitakavyoyafanyia kazi ili koberesha sekta
hiyo .
Aidha Prof. Mwatawala amewataka Wadau wa Tiba Asili na Tiba
Mbadala kuendelea kushirikiana na Chuo cha SUA na kutumia fursa mbalimbali
zinazopatikana ili kusaidia kutengeneza bidhaa zenye ubora, upatikanaji wa
masoko na mazingira bora.
Mhadhiri Mwandamizi kutoka SUA Dkt. Gay Merry Bakari ambaye ni
kati ya Watafiti ambao wameweza kuwasilisha kuhusiana na Tafiti ya Mmea
alioufanyia kazi na ambao umeleta matokeo chanya amesema alianza kufanyia
majaribio kwenye jeraha la Panya ili kuona kama dawa hiyo inaweza kuponya
vidonda na ikafanikiwa ambapo mpaka sasa zaidi ya watu 18 wamepona vidonda
kutokaa na dawa hiyo aliyoitengeneza kutokana na mmea dawa.
Akiwasilisha moja ya mmea unaofahamika kwa jina la Mvunjakongo
Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Mtafiti kutoka SUA David Credo amesema majani
ya mti huo hutumika kutengeneza dawa ya kudhibiti na kutibu kideri kwa kuku,
kudhibiti virusi katika mayai ya kuku, na kuongeza kuwa kemikali yake ikitumika
viwandani itasaidia kuzalisha dawa kwa ajili ya kuku.
Kongamano hilo la siku mbili ambalo lilianza Agosti 29 na
kuhitimishwa Agosti 30, 2022 limeambatana na Mdahalo kuhusiana na Usugu wa
vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa ambao umehusisha Wadau mbalimbali
wanaohusika na Tiba Asili wakiwemo SUA, Wizara ya Afya, TIRDO, GCLA, pamoja na
Waganga wa Tiba Asili kutoka mikoa yote Tanzania.
Maadhimisho ya 20 ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika
yameadhimishwa kitaifa mkoani Morogoro ambayo yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti
31, yakiwa na kauli mbiu “Miongo miwili ya Tiba Asili ya Mwafrika kuelekea
huduma za Afya kwa wote”.
0 Comments