SUAMEDIA

Serikali yashauriwa kufanya mapitio kuboresha viwango vya bidhaa zitokanazo na Rasilimali Misitu

 

Amina Hezron                      

Serikali imeshauriwa kufanya mapitio ya kuona namna bora ya kuboresha viwango vya bidhaa zitokanazo na rasilimali misitu hususani mkaa unaozalishwa kwa njia endelevu kutokana na bidhaa hiyo kutumiwa na watu wengi nchini.

Ushauri huo umetolewa Agost 26 mkoani Morogoro katika Warsha ya  Uthibitishaji wa Mazao ya Misitu Tanzania iliyoandaliwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili nchini Tanzania (TFCG) na Mtaalamu wa Uthibitishaji wa Misitu na Mazao ya Misitu kutoka Kampuni ya EFC Dkt. Severine Kalonga

Dkt. Severine Kalonga amesema takwimu zinaonesha asilimia 70 ya watanzania wanatumia nishati inayotokana na rasilimali misitu na hitaji la mkaa uliothibitishwa nchini bado ni mdogo kutokana na uwepo wa uzalishaji holela unaofanyika hivyo amewataka wauzaji kutambua thamani ya kuwa na mkaa uliothibitishwa ikiwemo uwepo wa ongezeko la gharama za uuzaji kutokana ongezeko la ubora .

“Nishati itokanayo na kuni ama mkaa ni nishati inayohitajika na kutumika na watanzania wengi hivyo bila kuweka viwango vya uthibiti wa namna ya kuzalisha mkaa kwa njia endelevu tutaendelea kupata changamoto ya uharibifu wa mazingira na misitu nchini”, alisema Dkt. Kalonga.

 Kwa upande wake Bw. Yuvenal Pantaleo ambaye ni Meneja Uthibitishaji kutoka Shirika la Mpingo Conservation and  Development Initiative (MCDI) amesema kwa upande wao tangu wamefanikiwa kupata uthibitishaji wa mbao kumekuwa na mabadiliko makubwa ya bei za mbao pamoja na kupata soko la uhakika la nje ya nchi kauli ambayo inaungwa mkono na Isaya Saitabau ambaye ni Meneja wa Msitu wa Jamii wa SULEDO.

Aidha Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaandaa Muongozo na Mkakati wa Taifa wa Matumizi endelevu ya Mazao ya Mkaa ili kuhakikisha mkaa unapovunwa na kutumiwa ni kwa maendeleo endelevu jambo litakalofanyika kwa kuzingatia mnyororo wa thamani kuanzia uvunaji mpaka hatua ya masoko.

Akieleza hayo  Mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii James Nshare amesema licha ya kuwepo kwa matumizi ya nishati zingine mbadala za gesi na umeme lakini bado watanzania walio wengi wanafanya matumizi ya nishati ya mkaa hivyo kutaka uvunwe na kutumiwa kwa njia endelevu  bila kuathiri misitu.

“ Kuna changamoto iliyopo ni vigumu sana kutofautisha mkaa uliovunwa kihalali na ambao haujavunwa kihalali  katika masoko hilo bado ni tatizo katika eneo la uthibiti lakini bado kupitia mkakati huu unaoandaliwa kuna mbinu ambazo zimeainishwa kama zitakwenda kusimamiwa zitasaidia kutatua changamoto hiyo”, alisema Nshare.

Aidha Nshare amefafanua kuwa suala la mkaa bado ni changamoto na linahitaji ushiriki wa wadau na sekta mbalimbali katika kuhakikisha unatumiwa kwa njia sahihi .

Warsha hiyo hiyo ya siku mbili ya Uthibitishaji wa Mazao ya Misitu iliyoandaliwa na TFCG kupitia mradi wa CoFoReST unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswizi(SDC) imeshirikisha wadau mbalimbali kama vile Shirika la Kuhifadhi Mpingo na Maendeleo (MCDI) TAFORI,SUA,TAMISEMI na Wizara ya Maliasili na Utalii.














Post a Comment

0 Comments