Na.Vedasto Gerorge.
Miradi ya Kilimo inayoanzishwa na Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA ikiwemo Mradi wa kuendeleza Kilimo safu za Milima ya Uluguru (UMADEP) imeendelea kuleta mafanikio kwa Wakulima ambapo wameendelea kuzalisha mazao kwa tija na yenye ubora baada ya kupatiwa Mafunzo na Teknolojia za kisasa kuhusu uzalishaji wa mazao ya chakula yakiwemo ya Mboga mboga na Matunda.
Wakizungumza na SUAMEDIA Wakulima wanaojishugulisha na kilimo
cha mazao mbalimbali akiwemo Semfilian Mahenge kutoka Kijiji cha Ndugutu na
Teresia Bonifasi wa kijiji cha Nyandira kata ya Nyandira Tarafa ya Mgeta wilaya
ya Mvomero mkoani Morogoro wamesema tangu kuanzishwa kwa Mradi wa Kilimo kwenye Milima ya Urugulu (UMADEP)
mwaka 1998 umeleta mabadiliko makubwa ya
kiuchumi kwenye familia zao.
“Huu Mradi tangu umekuja miaka ya tisini kiukweli ulikuja na
mambo matatu kwanza Mradi ulifanya tafiti
za mazao ya mboga mboga na matunda na tulipewa mbegu bora za kilimo kupitia Mradi huo yakiwemo Mafunzo ya
Ufugaji wa Mbuzi wa maziwa,
tunakishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa miradi
wanayotuletea kwa kweli Mgeta tumenufaika sana na mradi huu wa UMADEP”,
wamesema wanakijiji hao.
Aidha wamesema Mradi huo wa UMADEP uliwezesha upatikanaji wa
soko la mazao mbalimbali ikiwemo kuweka miundombinu ya barabara ili kuwawezesha
wakulima waliopo katika Kata tatu za Tarafa ya Mgeta kuweza kusafirisha mazao
yao.
Pia wamesema kabla ya ujio wa Mradi huo wa UMADEP katika
Tarafa hiyo hali zao za maisha zilikuwa duni kutokana na kutopata elimu juu ya ulimaji wa mazao kwenye
safu za Milima ya Urugulu ambapo walikuwa wakilima kwa mazoea hali iliyopelekea
Wakulima kuwa duni.
“Kiukweli kabla ya Mradi huu kuja Mgeta maisha yetu yalikuwa
ya chini kabisa kwa sababu tulizoea kufanya kilimo kisichokuwa na tija mazao
yetu yalikuwa ya kawaida na tulikosa mahala pa kuyauza, SUA tunawashukuru sana
Miradi kama hii tunaomba iendelee kuja
kwetu”, amesema Semfilian Mahenge Mkazi wa kijiji cha Ndugutu.
Kwa upande wake Msimamizi wa Kituo cha Kilimo na Wakulima
Mgeta William Shekilango kutoka Ndaki ya Kilimo, Idara ya Ugani na Maendeleo ya Jamii SUA amesema mpaka sasa
Mradi huo wa UMADEP unahudumia vijiji 28
vilivyopo katika kata tatu za Tarafa ya Mgeta wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.
“Mradi umewawezesha Wakulima kupata mafunzo ya kuweza
kulima kilimo cha mboga mboga na matunda
Chuo kiliweza kuwasafirisha wakulima kwenda mikoa mingine ambapo kule
walijifunza zaidi namna ya kulima mazao mbalimbali na walipo rudi kiukweli
walianza kulima wenyewe na sasa wanaendeleza kile walichojifunza juu ya
kilimo”, amesema Msimamizi huyo.
Pia Shekilango amesema licha ya kukuta shughuli za kilimo
milimani zikiwa zinaendelea lakini wakulima walio wengi hawakujua namna ya
kufanya kilimo hicho ambapo mazao yao yalikuwa yakisombwa na maporomoko ya maji
na kujikuta wakipata mazao machache kutoka mashambani.
Ameongeza kuwa kwa sasa wakulima wengi wanajua nini
wanachokifanya “kiukweli SUA naweza kusema kwenye Mradi huu wa UMADEP
tumefanikiwa kwa asilimia 100, sasa wanavuna mazao mengi na ukiangalia Wakulima
wengi wameweza kusomesha watoto, kujenga majumba hivi vyote vimetokana na uwepo wa Mradi ambao
ulikuwa unasimamiwa na SUA”.
“Chuo kimefanikiwa kuwatoa Wakulima kwenye kilimo cha mazoea
na sasa wanalima kwa tija na kimsingi
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kinatoa mafunzo na kimeweza kuwa karibu
na Wakulima wa Tarafa hii ya Mgeta na wamenufaika zaidi”, amesema
Shekilango.
0 Comments