SUAMEDIA

Wananchi waaswa kushiriki Yoga kuimarisha miili, kujikinga dhidi ya maradhi yanayosababishwa na mtindo wa maisha


NA. AYOUB MWIGUNE

Imeelezwa kuwa mchezo wa Yoga ni moja ya michezo yenye kuimarisha miili na kujikinga dhidi ya matatizo mengi yanayosababishwa na mfumo wa maisha.



Hayo yamebainishwa na Mkufunzi Michezo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Rashid Gumbwa wakati akizungumza na SUAMEDIA kuelekea Siku ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Yoga.

Awali akielezea kuhusu mchezo wa Yoga, Gumbwa amesema Yoga ni mazoezi ya kiroho na kimwili yenye asili katika falsafa ya Uhindi na  inajumuisha umoja wa roho na mwili, mawazo na matendo na uelewa kati ya mwanadamu na mazingira yanayomzunguka pamoja na mtazamo wa kiujumla wa afya ya binadamu. 

Aidha akielezea kuhusu faida ya mchezo huo  Gumbwa amesema moja ya faida kuu ya yoga ni kuimarisha karibu misuli yote  hata  ya ndani kabisa, kutokana na mchanganyiko wa mapumziko ya mwili na mvutano wa misuli.

Pamoja na hayo Gumbwa  amewaomba vijana wengi wanaotamani  kushiriki katika mchezo huo kutafuta ushauri kwanza wa Wataalam wa mchezo huo ili wasiweze kudhurika na baadhi ya mazoezi katika mchezo huo.

Ikumbukwe Desemba 11, 2014, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha mapendekezo na kukubali Azimio ambalo lilitambua Juni 21 kila mwaka iwe siku ya Kimataifa ya Yoga kwa kusambaza taarifa zaidi kuhusu faidi za Yoga duniani.





Post a Comment

0 Comments