Winfrida Nicolaus
Katika kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya mifugo pamoja na
mbolea ambazo zinatokana na mazao ya mifugo unakuwa wenye tija, Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo SUA kimeamua kuweka nguvu kubwa katika mafunzo kwa vitendo
kwa wanafunzi wote wa Shahada za Awali na Shahada za Juu pamoja na wananchi
wanaopata mafunzo ya muda mfupi chuoni hapo lengo likiwa ni kuzalisha wataalam
waliobobea ambao watatumia taaluma zao kwa ajili ya kusaidia jamii na Taifa kwa
ujumla
Msimamizi wa Shamba la Malisho katika Shamba la Mfano kutoka SUA Bw. Jontus Karoli akitoa maelekezo kwa wanafunzi walioshiriki katika mafunzo kwa vitendo, SUA. |
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Mashamba ya Mafunzo
kutoka SUA Bw. Roman Mfinanga wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye zoezi la
uvunaji wa mbegu kwa ajili ya malisho lililofanywa na Wanafunzi wa Stashahada
ya kwanza katika kozi ya Sayansi ya Mifugo na Uzalishaji chuoni hapo.
Bw. Mfinanga amesema mpango wa mafunzo kwa vitendo kwa
wanafunzi pamoja wananchi ambao wanafanya mafunzo ya muda mfupi chuoni hapo
kutoka maeneo mbalimbali nchini hata nje ya nchi kumeleta matokeo mazuri na
yenye tija kwenye
Tafiti hadi kwenye uzalishaji wa mazao hasa ya Mifugo kama
vile Maziwa, Nyama na Mbolea ambazo zinatokana na mazao ya mifugo na kuufanya
uzalishaji kuwa endelevu.
‘‘Tunategemea kutokana na mafunzo ya vitendo yanayotolewa
chuoni hapa wanafunzi wetu ambao watatoka kwenye chuo chetu wakimaliza masomo
yao yawezekana wengine watapata ajira Serikalini na wengine katika Taasisi
binafsi kule wanakoenda wataenda kutumia hizi taaluma ambazo wanazipata hapa
chuoni kwa ajili ya kuendeleza wananchi
wetu pamoja na Taifa, ’’ amesema Bw. Mfinanga.
Ameongeza kuwa kutokana mafunzo kwa vitendo yanayoendelea SUA
wananchi wategemee Taifa ambalo litakuwa na ongezeko kubwa la mazao ya mifugo
kwa tija lakini pia wananchi wenye uchumi mzuri kutokana na uzalishaji wa mazao
ya mifugo yenye ubora.
Kwa upande wake Msimamizi wa Shamba la Malisho katika Shamba
la Mfano kutoka SUA Bw. Jontus Karoli amesema mafunzo kwa vitendo
yanayoendeshwa SUA yamewasaidia wanafunzi kwa kiasi kikubwa wakiwemo Wanafunzi
wa Stashahada ya kwanza katika kozi ya Sayansi ya Mifugo na Uzalishaji ambao
wamefanikiwa kuingia kwenye hatua ya uvunaji wa mbegu kwa ajili ya malisho ya
mifugo ambayo waliyapanda wenyewe.
Amesema kupitia shughuli mbalimbali zinazotolewa na Chuo,
Wanafunzi wanakuwa wamejifunza kwa vitendo kuanzia uandaaji wa shamba mpaka
uvunaji lakini pia upatikanaji wa mbegu na malisho kwa ujumla hivyo inawajengea
uwezo na kuwa wataalamu bora katika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii
hasa kwenye Sekta ya Kilimo na Mifugo
‘‘Hivi sasa tupo katika zoezi la uvunaji wa mbegu za malisho
aina ya Lodes katika kuboresha afya za mifugo yetu hivyo tumepanda aina
mbalimbali za malisho au niseme majani kwa ajili ya mifugo na mpaka kufikia
hatua hii ya uvunaji wanafunzi ndio waliohusika zaidi katika shughuli yote hii
kuanzia uandaaji wa shamba mpaka mavuno yenyewe, na wao ndio wavunaji wameanza
kuvuna mbegu kwa ajili ya malisho baadae tutakuja malisho yenyewe hivyo mafunzo
kwa vitendo ndio muhimili mkubwa chuoni kwetu na lengo ni kupeleka mabalozi
wazuri kwa jamii mara baada tu ya kuhitimu’’
Naye mwanafunzi kutoka Stashahada ya Sayansi ya Wanyama na
Uzalishaji Grace Dickson ambaye yupo mwaka wa kwanza amesema kupitia shughuli
mbalimbali wanazozifanya chuoni zinawajengea uwezo wa kuwa wanataaluma bora kwa
ajili ya kuisaidia jamii na Taifa kwa ujumla lakini pia ni faida kwao wenyewe
kwa kuwa wameweza kufanya kwa vitendo.
Katika picha wanafunzi wa SUA wakishiriki katika Mafunzo kwa vitendo
KATIKA VIDEO
0 Comments