SUAMEDIA

Wakulima na Wafugaji wameshauriwa kuhamasishana na kushiriki kwenye mafunzo ya muda mfupi

 

Na: Farida Mkongwe

Wakulima na Wafugaji wameshauriwa kuhamasishana na kushiriki kwenye mafunzo ya muda mfupi yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) ili kuboresha kilimo chao.



Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Ugani cha ICE Dkt. Innocent Babili wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu mafunzo mbalimbali ya muda mfupi yanayotolewa na Chuo hicho kupitia Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Ndaki, Vituo, Taasisi na Shule Kuu zilizopo Chuoni hapo. 

Dkt. Babili amesema mara nyingi mafunzo hayo yanapotangazwa hufanyika baada ya kupatikana washiriki kati ya 20 hadi 30 lakini pia hujumuisha mafunzo yanayoandaliwa kutokana na maombi mahsusi ya mdau au wadau hata kama hawajafikia idadi hiyo.

“Mafunzo haya hutolewa kwa vitendo kwa asilimia 80 lengo likiwa ni kuwawezesha washiriki wetu wote waweze kujifunza bila kujali kiwango cha elimu waliyonayo, niwahakikishie kuwa sisi hatubagui, wakulima wote na wafugaji wakifika kwenye mafunzo haya watafaidika na kilimo chao kitabadilika”, amesema Dkt. Babili. 

Ameyataja baadhi ya mafunzo hayo yanayotolewa kwa siku nne hadi tano kuwa ni Uzalishaji na Utunzaji wa Malisho ya Mifugo, Utunzaji wa Udongo na Afya ya Udongo, Mafunzo ya Uzalishaji na Udhibiti wa Mende, Kilimo Biashara na Ujasiriamali, na Uzalishaji na Utunzaji wa Malisho ya Mifugo. 

“Mafunzo mengine tunayoyatoa ni Ufugaji wa Ng’ombe wa Maziwa, Udhibiti wa Viumbe-hai Waharibifu kwa kutumia Mfumo wa Vizuizi katika Mashamba ya Mpunga ya Umwagiliaji, Ufugaji wa Kuku, Ufugaji wa Samaki, na Ufugaji wa Nyuki”, amesema Dkt. Babili.




Post a Comment

0 Comments