SUAMEDIA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, imeridhishwa na uwekezaji uliofanywa na PSSSF katika Mradi wa Nguru Hills Ranch

 

Na.Vedasto George.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Jerry Silaa, imeridhishwa na uwekezaji uliofanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF)  kwenye Mradi wa Uendelezaji wa shamba la kunenepesha Mifugo na Machinjio ya kisasa ya  Nguru Hills Ranch ulioko Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Kufuatia kuridhishwa huko  Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Silaa ametoa maagizo matatu kwa Bodi ya Wadhamini ya PSSSF kuhakikisha inaendelea kusimamia mkataba wa uwekezaji katika machinjio hayo ya Nguru Hills kwa kushirikiana na wawekezaji wenza kwa lengo la kuhakikisha uzalishaji unaanza haraka iwezekanavyo na kupata tija iliyokusudiwa.

Pia Bodi ya PSSSF imeagizwa kuongeza kipengele kwenye makubaliano ya ubia na wawekezaji wenza kwenye machinjio hayo na kukiuzia Ngozi kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro Leather Industry Company Limited (KLIC) ambacho PSSSF imewekeza na hivyo kiwanda  kitapata uhakika wa Malighafi hali itakayopelekea kupata tija ya uwekezaji huo.

"Kamati pia inaagiza Bodi ya PSSSF kwa kushirikiana na wawekezaji wenza kuanzisha Program Maalum ya Elimu kwa Wafugaji ili kupata mifugo itakayokidhi viwango vinavyohitajika kwenye kiwanda," alisisitiza Mwenyekiti huyo.

Katika Mradi huo PSSSF inamiliki asilimia 39 ya hisa, huku wawekezaji wenza Kampuni ya Eclipse Investiment LLC ina hisa asilimia 46 na kampuni ya Busara Investment LLP yenye hisa asilimia 15.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Hosea Kashimba amesema Mradi upo katika hatua ya majaribio na makabidhiano kabla ya kuanza uzalishaji rasmi.



Post a Comment

0 Comments