Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimedhamiria kujenga uwezo wa ndani kwa kuendelea kuwekeza katika rasilimali watu, miundombinu na vifaa vya kisasa vya utafiti na ubunifu pamoja na kuimarisha mahusiano kati ya Taasisi za sayansi na teknolojia na Sekta ya viwanda ili kuchochea ubunifu na uvumbuzi nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Othman Masoud kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati akizindua wiki ya kitaifa ya Ubunifu kwa mwaka 2022 Jijini Dodoma.
“Matunda ya jitihada hizo za Serikali katika utekelezaji wa malengo hayo na hatua zinazochukuliwa yote yanabainika kupitia mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambapo jumla ya wabunifu 2,785 wameweza kuibuliwa mwaka huu na miongoni mwao wale walio mahiri zaidi ya 200 wameendelezwa na Serikali”, alieleza Mhe. Masoud.
Amesisitiza kuwa lengo kuu la Serikali ni kuwa Wabunifu na teknolojia zao walizozalisha ziweze kufikia hatua ya kupelekwa sokoni na kutumika na hivyo kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchangia pato la taifa.
Mhe. Masoud amesema katika kuhakikisha elimu ya sayansi na teknolojia inawekezwa kwa vijana ili kupata wataalamu wa fani mbalimbali kwa upande wa Zanzibar tayari wameshaanzisha mradi wa kujenga vituo 22 vya ubunifu wa sayansi Unguja na Pemba ambavyo vimeanza kutumika, mradi wenye thamani ya USD Milioni 35 zikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Amesema Serikali itaendelea kuwekeza, kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na teknolojia hapa nchini na kuhamasisha matumizi yake katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi katika masuala ya kijamii na kiuchumi.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua maonesho hayo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Adolf Mkenda amesema Maadhimisho hayo ya MAKISATU yanayofanyika kwenye mikoa 16 ya Tanzania ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya awamu ya sita ya kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na jamii.
“Wiki ya ubunifu ya kitaifa inahusisha majukwaa, majadiliano kuhusu maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini, mafunzo na semina kwa wabunifu ikiwemo elimu ya ujasiliamali, aidha mijadala hiyo inawahusisha Watafiti, Wavumbuzi, Wabunifu na Wadau mbalimbali wa ubunifu na Serikali katika kuweka mikakati mbalimbali ya pamoja katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii”, alieleza Prof. Mkenda.
Mhe. Mkenda amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya mashindano hayo ya MAKISATU jumla ya wabunifu 1,785 wameibuliwa na kutambuliwa na Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine na kwamba wabunifu mahiri 200 wanaendelezwa na wizara kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH ili ubunifu wao ufikie hatua ya kuwa bidhaa na kuingia sokoni na kuongeza fursa za ajira na kipato cha vijana nchini na tayari bunifu 26 zimeingia sokoni.
Amesema katika mashindano hayo ya mwaka huu 2022 jumla ya wabunifu 86 wamepatikana kutoka katika makundi yote nchi nzima ili kushindanishwa na mwisho yaani siku ya kilele watapatikana washindi ambao watatunukiwa zawadi na bunifu zao kuendelezwa na Serikali kupitia COSTECH.
Akitoa neno la shukrani Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP ambao ndio wafadhili wakuu wa MAKISATU Bi. Christine Musis amesema wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kujenga utamaduni wa Ubunivu na uvumbuzi nchini.
“Niko hapa kama mdau mkubwa wa serikali katika kusaidia kuchochea ubunifu kwa vijana wa kitanzania na kuwapa kianzio cha msaada wanaohitaji kupiga hatua kutoka mawazo, sampuli kifani hadi kufikia hatua ya kufika sokoni ili wawe injini ya ukuaji na maendeleo nchini Tanzania”, alisisitiza Bi.Musis.
Awali kabla ya kufungua Wiki hiyo ya kitaifa ya Ubunifu Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Othman Masoud na viongozi wengine wa Wizara na Serikali walitembelea mabanda mbalimbali yanayoonesha bunifu na teknolojia mbalimbali ikiwemo banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na kuvutiwa na maelezo ya namna panya wanavyoweza kutambua makohozi na mtu mwenye TB na kugundua mabomu maelezo yaliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Prof. Raphael Chibunda na baadae kupata maelezo kutoka kwa Prof. Gerald Misinzo na kuona namna Gari ambalo ni Maabara inayotembea ya SUA linavyofanya kazi.
0 Comments