Katika kuhakikisha Wagaga wengi wa tiba asili nchini wanauza dawa bora na salama kwa binadamu,Wanyama na mazingira, Mkemia Mkuu wa Serikali amepunguza gharama za upimaji wa dawa hizo ili zipimwe na kusajiliwa kisheria.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Maabara ya chakula na dawa kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Shimo Peter wakati akizungumza na waganga wa tiba asili kwenye warsha ya wadau wa tiba asili na tiba mbadala kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania iliyoratibiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia mradi wake wa VaSPHAD.
“Kumekuwa na maombi ya muda mrefu ya waganga wa tiba asili kuomba Mkemia Mkuu wa Serikali kupunguza gharama za upimaji wa dawa ili waweze kusajiliwa kwa hiyo Mkemia Mkuu ameliangalia na hatimae amepunguza gharama kutoka dola za kimarekani 311 hadi kufikia dola 152 ambayo ni karibu nusu ya gharama za awali” , alisema Dkt. Shimo.
Amefafanua kuwa ili kuweza kupimiwa kwa kutumia punguzo hilo kuna taratibu ambazo wanapaswa kuzifuta Waganga hao ambazo ni kujaza fomu kutoka Baraza la Tiba asili na tiba mbadala au waratibu wa tiba asili kutoka wilayani au mkoani na kwamba kinyume na hapo watajikuta wanalipa zaidi ya dola 500 kwa dawa moja.
Amewataka kufikisha taarifa hizo kwa wenzao kote nchini ili waweze kutumia fursa hiyo waliyoiomba kwa muda mrefu mara kwa mara iliyotolea na Mkemia Mkuu wa Serikali ili waweze kuuza dawa zenye viwango na ubora utakaowawezesha kufikia soko la ndani na nje ya nchi.
Amewasisitiza watoa huduma kuzalisha dawa asili kufuata kanuni na miongozi ya uzalishaji bora na salama, kutumia kemikali kufuata Sheria ya Kemikali namba 3, ya mwaka 2003 inayosimamiwa na GCLA na kupata mafunzo ili kuweza kutambua njia salama za matumizi ya kemikali.
Awali Mkuu wa Mradi wa GRILL na VaSHPARD kutoka SUA Dkt. Faitha Mabiki amesema lengo la warsha hiyo ni kuendeleza jitihada za Chuo na Serikali katika kubadili tabia za namna wanavyotengeza dawa za asili na wanavyotoa huduma kwa jamii.
“Kwa kuwa toka tumeanza mradi tumeona mabadiliko makubwa sana katika utengenezaji wenu wa dawa na utoaji wenu huduma hivyo tunaamini warsha kama hii inayowakusanya pamoja kutoka mikoa mbalimbali na kupata mafunzo kutawasaidia zaidi kutoka kwenye kufanya kazi kwa mazoea kwa kubadili tabia na hatimae kutengeneza dawa asili zenye viwango vinavyokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi”, alieleza Dkt. Mabiki.
Mtafiti huyo amesema kwenye warsha hiyo pia watatoa matokeo ya vipimo vya dawa zao mbalimbali walizozipeleka SUA kwa ajili ya vipimo vilivyobaki kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye aliomba wataalamu wa SUA kusaidia kuzipima na kuwapatia majibu kila mmoja na kumshauri mambo ya kufanya ili kufikia ubora unaotakiwa.
Amesema dawa kutoka nje ya nchi zinazoonekana zinapitia michakato mingi ili kuweza kupata nembo za ubora na mamlaka za nchi hizo na kimataifa ndio maana SUA na Serikali kupitia Mkemia Mkuu wa Serikali wanashirikiana ili kuwawezesha waganga hao waweze kulifikia kirahisi soko la nje.
Amewataka kuendelea kushirikiana miongoni mwao na kuwasiliana katika masuala mbalimbali kwa kuwa kila mmoja ana uelewa tofauti kutokana na mazingira wanayotoka na itawasaidia kupeana ujuzi na kuongeza uelewa zaidi badala ya kila mmoja kufanya mambo yake kwa siri.
Akizungumza kwa niaba ya Waganga wengine walioshiriki warsha hiyo Dkt.Flavian Nyakeji kutoka Njombe amemshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kusikia kilio cha gharama kubwa za upimaji wa dawa na kuahidi kuitumia vyema fursa hiyo ili kuweza kufikia viwango.
“Suala la gharama kubwa za upimaji limekuwa kilio chetu cha muda mrefu maana wengi wetu kweli tunazo dawa za asili nzuri na zinatibu lakini hatuna uwezo wa kulipa dola 500 zaidi ya kupima dawa moja ili tusajiliwe lakini sasa kwa gharama hiyo ya shilingi dola 152 tutahakikisha tunapima dawa zetu kwa faida yetu, jamii na wateja wetu”, alisema Dkt.Nyakeji.
Katika warsha hiyo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo aina za viungo vya kemikali kwenye mimea,utengenezaji wa kemikali, kazi za kemikali kwenye mimea na utabibu, athari za sumu kuvu katika afya na biashara, namna ya kupunguza na kuzuia sumu kuvu kwenye bidhaa, Matatizo ya kiafya yanayosababishwa na vimelea, mambo hatari yanayochangia kuwepo kwa vimelea pamoja na mada zingine nyingi.
Warsha hiyo imewakutanisha waganga wa tiba asili kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania hususani wale ambao walipeleka dawa zao kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya vipimo na zikabaki ili waweze kupewa majibu ya dawa zao.
0 Comments