Na.Vedasto George.
Wakulima wa mbogambona na matunda wametakiwa kuendesha kilimo hicho kwa kufuata kanuni bora za kilimo ili waweze kuzalisha kwa tija na kuweza kushindana kwenye soko la ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja wakati wa ufungaji wa Mradi wa miaka mitano na nusu wa FEED THE FUTURE TANZANIA MBOGA NA MATUNDA ambapo umewezesha kutoa mafunzo kwa wakulima wa mboga mboga na matunda zaidi ya 180,000 kutoka wilaya nne za mkoa wa Morogoro .
‘Tuzalishe lakini tuzalishe kibiashara lakini tuhakikishe pia tunazalisha kwa tija yaani kama unatakiwa kufuata taratibu za kanuni bora za kilimo ni sasa na hii itatusaidia kuacha kuzalisha kiolela na mazao ya ovyo ambayo ayawezi kuingia sokoni ,huu mradi umewezesha wakulima wetu 183,709 ambao wamepata mafunzo mbalimbali juu ya ulimaji wa mazao ya mboga mboga na matunda”, amesema Bi. Mariam.
Aidha Mtunguja amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri ambazo zimenufaika na Mradi wa mboga mboga na matunda kuendelea kutenga bajeti kwa maafisa ugani ili waweze kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ikiwemo kuwawezesha kupata mbegu bora ambazo zitaweza kutoa mazao yenye tija kwa mkulima.
Pia ameongeza kuwa serikali imeendelea kuchukua jitahada za makusudi za kutafuta masoko nje ya nchi ili wakulima wanaozalisha mazao yao kutoka shamba waweze kupata soko la uhakika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa FEED THE FUTURE TANZANIA MBOGA NA MATUNDA, Antonio Coello amesema Mradi huo umetekelezwa kwa mafanikio makubwa katika wilaya 26 za mikoa ya Morogoro, Mbeya, Songwe,Iringa na Njombe na wilaya 10 za Tanzania Visiwani katika visiwa vya Unguja na Pemba.
“Mradi unatumia mfumo wa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuweza kutoa huduma za kilimo bora ,Teknolojia za kilimo pamoja na elimu ya lishe ili kuweza kuwafikia watanzania maelfu kwa maelfu wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani katika uzalishaji wa mazao ya mboga mboga na matunda”, amesema Mkurugenzi huyo
Naye Mkurugenzi Msaidizi na Mwalishi wa USAID Stephen Mruma ameeleza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Mradi huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 hadi sasa ambapo umefikia tamati mwaka 2022.
Mruma amesema Mradi huo wa Mbogambona na Matunda umeweza kuwafikia watu zaidi ya 400,000 kwa Tanzania nzima na wote wamefundishwa kanuni bora za kilimo cha mboga na matunda ikiwemo kutafutiwa masoko ambayo wakulima wataweza kuuza mazao yao na kuweza kupata kipato cha kuendeleza familia zao.
Nao wakulima ambao ni wanufaika wakubwa wa mradi huo akiwemo Abel Mchome pamoja na Anania Masimile kutoka Kampuni ya Balton Tanzania wamesema kwa kipindi chote cha miaka mitano na nusu Mradi umekuwa ukiwaunganisha na wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi za fedha , Wauza pembejeo za kilimo na Wafanyabiashara wakubwa ambao wamekuwa wakinunua bidhaa zao .
“Tumenufaika sana na mradi huu kwanza walipokuja walitupa elimu na njia bora za kufanya kilimo cha mboga na matanda na sisi tukaanza kulima tuliona mafanikio mazao yalitoka mengi baada ya kuzalisha ikabidi watutafutie soko na kutuunganisha wa taasisi za fedha kwa ajili ya kutuwezesha kupata mikopo, kwa kweli mradi huu unaisha lakini maarifa tuliyopewa tutayaendeleza”,alisema Abeli Mchome mkulima wa Mboga na matunda kutoa Halmashauri ya wilaya ya kilosa.
Katika Video
https://www.youtube.com/watch?v=kHnwFtUZ2GY
0 Comments