Winfrida Nicolaus
Kutokana
na tafiti mbalimbali duniani zinazoonesha kwamba watu wa rika mbalimbali
hujifunza na kuzingatia zaidi mafunzo iwapo yatatolewa na watu wenye umri,
jinsia na shughuli zinazofanana, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kimeendelea kuwajengea uwezo wanafunzi toka kwenye kozi mbalimbali chuoni hapo
ili waweze kusaidia kutoa elimu ya jinsi ya kupambana na kudhibiti magonjwa
sugu yasiyoambukiza (MSY) pamoja na Ukimwi.
Hayo
yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi, Kurugenzi ya Shahada za Awali katika Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo SUA Dkt. Alex Matofali wakati
akifungua mafunzo kuhusiana na namna bora za kudhibiti na kupambana na magonjwa
sugu yasiyaambukiza (MSY) Pamoja na Ukimwi kwa baadhi ya wanafunzi chuoni hapo
ambao wataenda kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii pamoja na wenzao.
Dkt.
Matofali amesema kuwa magonjwa sugu yasiyoambukiza Pamoja na Ukimwi yamekuwa
yakiuchangia ulemavu (disability) na vifo vingi kwa vijana na watu wa rika
mbalimbali na madhara hayo yameongezeka sana katika miaka ya karibuni ambapo
kwa mwaka 2016/2017 imebainika kwamba sehemu kubwa ya maambukizi mapya ya VVU
yanatokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 – 23 kundi ambalo wengu wao
kwa sasa wapo vyuoni.
Aidha
amesema hivi sasa familia na serikali zimekuwa zikiwekeza sana katika suala la
elimu ya juu, lengo na madhumuni ya uwekezaji huo ni kuhakikisha wanafunzi
wanapata ujuzi ili waweze kusaidia familia zao na kuchangia katika maendeleo ya
taifa kwa ujumla hata hivyo pamoja na dhamira zao nzuri iko hatari kwa ndoto
hiyo kufutika kutokana na athari za VVU/UKIMWI na Magonjwa sugu yasiyoambukiza (MSY).
“Unajua acha tu niseme magonjwa sugu yasiyoambukiza kwa sasa yamekuwa ni
hatari sawa na Ukimwi na yamekuwa yakisababisha vifo vingi pamoja na ulemavu na
kwa bahati mbaya zaidi magonjwa sugu yasiyoambukiza yamekuwa yakisababishwa kwa
sehemu kubwa na mienedo ya maisha kuanzia umri mdogo. Ni kwa msingi huo
imelazimu kuanza kutoa elimu kuhusu magonjwa tajwa kwa lengo la kuchukua hatua madhubuti
mapema”. Amesema Dkt. Alex Matofali.
Kwa
upande wake Dakatari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka katika Hospitali ya
SUA Dkt. Elimwidim Swai amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani
(WHO) watu zaidi ya Millioni Moja wanaathirika na magonjwa yanayoambukizwa kwa
njia ya Ngono (STI) kila mwaka na hivyo wameamua kutoa elimu kila wakati kwa
jumuiya ya SUA ili kupunguza maambukizi kwa kizazi hiki na kijacho.
Ameyataja
madhara yatokanayo na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya ngono kuwa ni pamoja
na kushindwa kuzaa, mimba kutunga nje ya kizazi kwa wanawake, kupata saratani,
wanawake kujifungua kabla ya wakati (premature), au kujifungua mtoto
aliyefariki.
“Ili kujilinda sisi pamoja na wenza wetu
katika magonjwa haya yanayoambukiza kwa njia ya ngono hususani ukimwi tunapaswa
kuwa waaminifu kwa wenza wetu yani
tusiwe na mpenzi zaidi ya mmoja lakini pale inapobainika mmoja wetu ameathirika
na ugonjwa huu tujitahidi kufuata masharti ya wataalamu wa afya na kutumia
kinga kwa usahihi lakini pia tujiepushe kushirikiana vitu vyenye ncha kali kama
nyembe” Amesema
Dkt. Swai.
0 Comments