Na Amina Hezron
na Calvin Gwabara, Dodoma.
Matokeo ya
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine yanaonyesha kuwa shughuli za
kibinadamu zinazofanyika katika maeneo ya dakio bonde la maji chini ya ardhi la
makutupola ambalo ndio chanzo kikuu cha maji cha Jiji la Dodoma zinauwezekano
mkubwa wa kuathiri uwepo wa chanzo hicho cha maji endapo jitihada za makusudi
hazitachukuliwa kulinda chanzo hicho.
Hayo yameelezwa
Jijini Dodoma na Mtafiti kutoka katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
Prof. Japhet Kashaigili katika warsha ya mawasilisho ya matokeo ya utafiti
ulioangalia maji chini ya ardhi katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara
mbele ya wadau wa chanzo hicho cha maji uliofanywa na Watafiti wa SUA kwa
kushirikiana na Chuo Kikuu cha Cardiff na Chuo Kikuu cha Jiji la London
Uingereza.
Prof.Kashagili
amesema kuwa bila kukaa kwa pamoja kujadiliana namna bora za kulinda eneo hilo
sasa chini ya mpango wa upangaji wa Makazi, athari yake itakuwa kubwa ambayo
itapelekea kulipa pesa nyingi huko baadae.
“Kuna haja ya
kuyaangalia haya mapema ikiwezekana bonde hili litangazwe lote kwenye Gazeti la
Serikali kuwa sehemu ya hifadhi ya bonde na liangaliwe kwa upekee wake ili
kuzuia shughuri za kibinadamu ambazo zinaweza zikaathiri eneo lile kutokana na
umuhimu wake kwa kuwa kimsingi ukiangalia tathimini ya maji
mbalimbali ambayo yametokana na vyanzo mbalimbali karibuni zaidi ya
asilimia 90 za maji ya mji huu wa Dodoma yanatoka pale ”, ameeleza Prof.
Kashaigili.
Aidha Prof
Kashaigili ameongeza kuwa kwa kuwa mvua kwa miaka ya karibuni hazijawa kuwa
kufikia zile za El nino zinaweza tumiaka mbinu zingine ambazo zimetumiwa nan
chi zingine duniani za kuchimba visima na kuruhusu maji kujaa kwenye eneo hilo
na kuyaacha yaingie kwenye mwamba huo ardhini na kisha kuweza kuyatumia
kupelekwa kwenye maeneo mengi zaidi ya jiji la Dodoma.
“Inawezekana
haya maji tukayatathimini ubora wake lakini tukayaruhusu yakakaa juu ya
ardhi kwakuweka mazuio mbalimbali ili yaweze kunywea kuingia ardhini
jambo ambalo nchi mbalimbali zimefanya hivyo na zimefanikiwa kuondoka na adha
zilizopo za upatikanaji wa maji”, alifafanua Profesa Kashaigili.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji Dkt George Lugomela
ameeleza kuwa kwa siku jijini Dodoma linahitajika mita za ujazo 133,845
upatikananji wake ni mita za ujazo 66,600 kwa siku ambayo ni kama nusu ya
mahitaji na hii ni kutoka na ongezeko la watu katika jiji hilo.
“Serikali tayari
imeweka mikakati Madhubuti katika kuhakikisha changamoto hii inatatuliwa ikiwemo
kuchujenga bwawa la FAKWA lakini mkakati wa haraka ni kuchukua maji mita za
ujazo 100,000 kwa siku kutoka bwawa la Mtera ambazo ukichanganya na zile 66,600
za sasa unapata mita za ujazo 166,600 ambazo zitakuwa na uwezo wa kukidhi
kabisa mahitaji ya Jiji lote la Dodoma” alifafanua Dkt. Lugomela.
Hivyo amesema
kuwa matokeo ya Utafiti huo ni muhimu sana na yatatumiwa na Wizara katika
kuwezesha kutazama namna ambavyo itawezekana kutatua changamoto hiyo ya maji
kupitia chanzo cha Makutupola tofauti na ilivyo hivi sasa.
Nae Mtafiti Mkuu
wa mradi huo Prof. Richard Tayrol kutoka katika Chuo Kikuu cha Jiji la
London nchini Uingereza amesema kuwa mradi huo unatekelezwa katika nchi tatu
ambazo ni Tanzania, Nigeria na Ethiopia pamoja na malengo mengine lakini pia unalenga
kuangalia namna maji yaliyo chini ya ardhi yanavyoweza kuchangia katika kuondoa
umasikini.
Ameeleza kuwa
maji ya chini ya ardhi hayawekewi mkazo sana kama ilivyo kwa maji ya juu ya
ardhi hivyo ameishauri Serikali kuwekeza katika maji yanayopatikana chini ya
ardhi kakuwa kuna maji mengi kuliko haya tunayoyaona juu ya ardhi yanayopita
kwenye mito na maziwa.
“Naishauri
Serikali kuwekeza nguvu, muda pamoja na kuwajengea uwezo watu wake katika
kutambua rasilimali hii ya maji yaliyopo chini ya ardhi maana katika fani ya
hydrolojia, kwani itasaidia katika kukabiliana hata na mabadiliko ya tabia nchi
na kuchangia katika matumizi mbalimbali kama vile Kilimo,Viwanda na matumizi ya
nyumbani ”, alisema Prof. Tayrol.
Naye mmoja
ya wakulima ambao wamepata nafasi ya kuhudhuria warsha hiyo kwa niaba ya
wakulima wengine Dkt. Huruma Msuya ameishauri Serikali kutenga maeneo maalumu
kwa ajili ya misitu kilimo cha mbogamboga na matunda kwaajili ya kulisha
miji jambo litakalosaidia mji kuwa na sehemu ya kupumulia.
“Tusifanye makosa
kama yaliyofanyika kwenye Jiji la Dar Es Salaam ambapo mji umekuwa tu kutoka
Kariakoo mpaka Kibaha bila kuwa na maeneo yenye mashamba na Misitu, mji
usikue tu kuwe na miji midogo midogo pembeni ya mji mkubwa ambayo nayo itakuwa
imeendelea itakuwa inapata maji huko huku kupunguza hali ya upatikanaji wa maji
kutoka upande mmoja”, alisema Dkt. Msuya.
Matokeo ya tafiti
yaliyowasilishwa ni matokeo ya utafiti iliyofanyika kwa miaka mitano na
mradi wa GroFutures ulioanzishwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa
kushirikiana na Chuo cha Cardiff kilichopo nchini Uingereza pamoja na
Chuo Kikuu cha jiji la London nchini Uingereza .
0 Comments