Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja
Kadogosa amesema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Makutupora-Tabora
utagharimu Sh4.606 trilioni huku ukitarajiwa kutumia miezi 42 ikiwemo miezi
minne ya majaribio.
Treni zitakayotumia reli hiyo zitakuwa na mwendokasi wa
kilomita 160 kwa saa ambapo zitatumia saa sita kutoka Dar es Salaam hadi Tabora
kwa treni ya abiria huku za mizigo zikitembea kilometa 120 kwa saa.
Kadogosa amesema hayo leo Jumanne Aprili 12, 2022 katika
uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa reli hiyo unaofanywa na Waziri wa Ujenzi na
Uchukuzi,Profesa Makame Mbarawa.
Amesema makadirio ya majaribio yanategemea kuwa muda wa chini
sana utakuwa miezi minne, lakini yanaweza kwenda hadi zaidi ya miezi hiyo.
“Kwa hiyo tunategemea mradi huu unaoanza saa hizi, utakamilika
Oktoba 2025, hii inajumuisha usanifu na ujenzi kwa mkandarasi. Wakati anasanifu
kuna baadhi ya nyumba zitapitiwa ila wote watapatiwa haki zao,”
Amesema mkandarasi amashapewa aina ya reli ambayo inayohitaji
na si yeye kuleta kile ambacho hakitakiwi.
“Itakuwa na vivuko vya kutengenisha reli na barabara kwa
kuondoa muingiliano wa barabara na reli, hii ikiwa na maana kuwa ikiwa yeye
atakuwa chini treni itapita juu au yeye akiwa juu treni itapita chini jambo
hili litafanya usalama kuwa wa juu”
Amesema katika ujenzi huo, madaraja makubwa 32 yanatarajiwa
kujengwa na vivuko vya juu 12 na vya chini 15 huku vivuko vya watembea kwa
miguu, mifugo na wanyama vikiwa 49.
“Vivuko hivi vinamaana kwa sababu reli hii haitaruhusu mtu
kupita juu kwa ajili ya usalama, tutazungushia wigo reli yote,”
Treni hiyo itakapoanza kazi itakuwa na vituo nane Manyoni,
Itigi, Kazikazi, Tula, Malongwe, Gaweko, Igalula na Tabora.
“Niwaambie tu, hatujengi stesheni hapa Tabora, tutajenga
‘shopping mall’, sehemu ya maduka makubwa, migahawa, tutakuwa na sehemu ya wafanyabiashara
wadogo. Nina imani kuwa pale ndiyo itakuwa sehemu mnakutania,” amesema
Kadogosa.
CHANZO MUUNGWANA BLOG
0 Comments