Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai amesema chanjo ya ugonjwa wa homa
ya sotoka ni mkombozi kwa wafugaji wa Kongwa ambao wametaabika kwa muda mrefu.
Pia, Ndugai amewataka
wataalamu kwenda mbele zaidi kwa kuanza kutazama uwezekano wa kutengeneza
chanjo ya Ukimwi ili wananchi wafurahie maisha.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ndugai kuonekana hadharani tangu
alipojiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge Januari 6 mwaka huu, huku wengi wakitaka
kujua aliko baada ya kutoonekana bungeni.
Ndugai ameonekana hadharani jana Jumatatu Aprili 11, 2022
katika uzinduzi wa chanjo ya mifugo ya ugonjwa wa homa ya sotoka uliofanyika
katika Wilaya ya Kongwa.
Akizungumza mbele ya wafugaji katika uzinduzi huo uliofanywa
na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, Ndugai amesema kwa watu wa Kongwa
ni furaha na neema ambayo wanapaswa kuishukuru Serikali ya awamu ya sita.
Spika huyo wa zamani amesema kwa namna yoyote ufugaji wa mbuzi
ulishashindikana katika wilaya hiyo lakini uwepo wa chanjo unakwenda kuwainua
wafugaji akiwemo yeye kuwekeza zaidi kwenye mbuzi.
"Nampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali
yake kwa kutukumbuka watu wa Kongwa, Mheshimiwa Waziri tupelekee salamu na pongezi
nyingi sana,"amesema Ndugai.
Katika hatua nyingine ameahidi kufanya kazi na kushauriana na
Waziri Ndaki kwani amepangwa katika kamati ya Kilimo Mifugo na Maji ambayo ipo
chini ya Wizara hiyo.
CHANZO MUUNGWANA
0 Comments