Calvin Gwabara
Morogoro.
Serikali imeahidi
kusambaza na kuendeleza mfumo wa uhifadhi na usimamizi shirikishi wa misitu ya
asili kwenye wilaya zote nchi nzima ili kulinda misitu hiyo na kuwezesha vijiji
kunufaika na uwepo wa mistu kwenye maeneo yao baada ya mbinu hiyo kuonesha
mafanikio makubwa kwenye Vijiji vya awamu ya kwanza na ya pili ya mradi.
Afisa Misitu Mkuu Idara ya Uratibu wa Maliasili na Mazingira kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bw. Sanford Kway akizungumza na waandishi wa habari
Ahadi hiyo
imetolewa na Afisa Misitu Mkuu Idara ya Uratibu wa Maliasili na Mazingira
kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bw. Sanford Kway
wakati akiongea na waandishi wa habari nje ya mkutano wa uwasilishwaji wa
matokeo ya tafiti saba zilizofanywa na wadau mbalimbali katika maeneo ya
yanayotekeleza Mradi wa CoFOREST ambao unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu
ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania
(MJUMITA).
“Kweli
tunatambua kuwa mradi unaisha na mafanikio haya kama serikali hatutamani
yaishie hapa ndio maana kwenye awamu ya tatu ya mradi tumekubaliana kwamba
watekeleze kwenye Kijiji kimoja kimoja kwenye kila wilaya mpya za mradi ili iwe
sehemu ya wao kuwajengea uwezo wataalamu wa halmashauri kuelewa vyema mfumo huu
ili nao wasambaze kwenye vijiji vingine na kweli tunaona kuna uendelevu”
Alisema Bw. Kway.
Amesema
progamu hiyo ina manufaa makubwa kwa Serikali kwa sababu kuwezesha waananchi
kusimamia ile misitu yao na wao kupitia motisha wanayoipata kuna sababisha wao
kuwa walinzi wazuri maana wanaona kuna manufaa wanayapata hivyo hawawezi kuacha
iharibiwe bali watailinda na kuivuna kwa uendelevu.
Magunia ya Mkaa yaliyotayarishwa kwenda sokoni
Afisa Misitu
Mkuu huyo Idara ya Uratibu wa Maliasili na Mazingira kutoka TAMISEMI amekiri
kuwa katika wilaya tatu za awamu ya kwanza za Mkoa wa Morogoro wananchi wameweza
kutumia kile wanachokipata katika kufanya shughuli nyingi za kijamii kama vile
kujenga miundombinu ya shule, zahanati, ofisini za vijiji na Bima za Afya
ambayo pengine Serikali isingeweza kuyafanya kwa haraka hivyo.
“ Tunafahamu
kuwa vijiji kupitia mapatoa yao wanarejesha asilimia 10 ya mapato kwenye
halmashauri ambazo baadae kiasi hutakiwa kurudishwa kwenye vijiji au kutumiwa
na maafisa wa halmashauri kufanya shughuli za ugani kwenye vijiji lakini hii
imekuwa changamoto kwenye vijiji vingi vya mradi huu na Serikali imeliona na
kuliwekea mkakati mzuri ambao ukikamilika utasaidia halmashauri kuzirejesha kwa
wakati “ Alifafanua Bw Kway.
Kwa upande
wake Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti wa Matumizi ya Misitu ya Taasisi
ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) Dkt. Chelestino Balama amesema kuwa yale
yote yanayofanywa na mradi huo wa CoFOREST yanapata ushauri kutoka TAFORI maana
wao ni sehemu ya wajumbe wa kamati ya ushauri katika utekelezaji wake.
Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti wa Matumizi ya Misitu ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) Dkt. Chelestino Balama akitolea ufafanuzi baadhi ya mambo juu ya mradi huo
Amesema
mawasilisho hayo ya tafiti saba yanatokana na ushauri wao kuwa wakati mradi
ukiendelea lazima kufanyike tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia kupatikana takwimu
sahihi na ushahidi wa kisayansi ambao utawezesha maamuzi yoyote yatakayofanywa
na Serikali.
“Mradi huu
kama utasimamiwa vizuri unaweza kuwa suluhisho la changamoto za uharibifu wa
misitu ya asili iliyo kwenye ardhi za vijiji maana tumetembelea kwenye vijiji
vyote vinavyotekeleza mradi na tumeona kwa macho yetu namna walivyoweka mfumo
mzuri wa uvunaji ambao kweli ni endelevu lakini kubwa tunaomba kuwepo kwa
mahusiano mazuri na misimamo kwa viongozi wa vijiji katika utekeelzaji ili
kuwepo na uendelevu” amesema Dkt. Balama.
Magogo ya miti yakitayarishwa kwa ajili ya kutengeneza mkaa
Mradi huu
unaendeshwa TFCG na MJUMITA kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa
Misitu ya Jamiii (USMJ) unatekelezwa chini ya Mradi wa kuleta Mageuzi katika
Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) Mradi wa kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu
ya Misitu (CoFOREST) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).
0 Comments