SUAMEDIA

Ili nchi ipange bajeti katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi na elimu jitokezeni kwenye zoezi la Sensa - Prof Chibunda

 

Na Gladness Mphuru

SUA

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema ili nchi iweze kupanga na kutenga bajeti kulingana na idadi ya wahitaji, kwenye sekta mbalimbali kama sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kujua uhitaji wa wakulima na katika sekta ya Elimu ni muhimu watu wakajitokeza katika zoezi la sensa

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani ofisini SUA-Morogoro

Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda Aprili 20, 2022 ofisini kwake Kampasi ya Edward Moringe Sokoine mkoani Morogoro, wakati akizungumza na waandishi wa habari  kwa lengo la uhamasishaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kuanza Agosti 23, mwaka huu.

“Kama ambavyo mheshimiwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan amekuwa akihimiza hakuna kitu muhimu kama zoezi hili, na hili sio la Tanzania pekee ni zoezi linalofanyika katika kila nchi duniani kwa vipindi mbalimbali walivyojipangia ili kuweza kupata takwimu sahihi kwenye kupanga maendeleo ya nchi husika” Amesema Prof. Chibunda

Ametoa wito kwa watanzania wote hususan kwa wanajumuiya wa SUA wafanyakazi na wanafunzi hasa vijana ambao wanashiriki zoezi hili kwa mara ya kwanza kushiriki kikamilifu kwa sababu ndio nguvukazi kubwa kwa taifa.

“Na vilevile nishauri katika baadhi ya jamii za nchi yetu kumekuwa na tabia ambazo sio nzuri na potofu walemavu wa viungo wamekuwa hawatolewi hadharani ili nao waweze kuhesabiwa, ni muhimu watu wote kuhesabiwa hususani wenye mahitaji maalumu ijulikane ni wangapi ili nchi iweze kuwahudumia”

Prof. Raphael Chibunda, amesema yeye yuko tayari pamoja na familia yake kushiriki katika zoezi muhimu la sensa ya watu na makazi, zoezi litakalo rahisishia nchi kupanga mipango ya maendeleo.

Kauli mbiu ya Sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 inasema “Sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo shiriki kuhesabiwa tuyafikie maendeleo ya Taifa”

Post a Comment

0 Comments