Gladness Mphuru
SUA
Mkuu wa Chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole kilichopo Bagamoyo Bw.
Sinani Simba, amesema watashirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kwa sababu mbali na kubobea katika utoaji bora wa elimu pia inachangia katika
kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana kupitia kilimo.
Bw. Simba ametoa kauli hiyo leo tarehe 21, Aprili 2022 katika
Kampasi ya Edward Moringe Sokoine mkoani Morogoro, wakati wa ziara yao ya
kukitembelea chuo cha SUA akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa SUA
ambapo amepata mapokezi kutoka kwa mwenyeji wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda.
Mkuu huyo wa Chuo cha Kaole, amesema kuwa SUA mbali na kutoa
elimu kwa wanafunzi pia imetoa fursa kwa wananchi hususan vijana, kupitia kituo
atamizi kwa ajili ya vijana wajasiriamali kinachoitwa PASS AIC SUA, ambao wanapatiwa
elimu, wanapewa maeneo ya kulima ndani ya chuo pamoja na mikopo nafuu.
“atamizi hiyo inaonesha dhamira chanya ambayo inaonesha kwamba
SUA mmepania katika kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana, lakini pia
mnawaonesha wanafunzi kufanya kwa vitendo wakitoka hapo wanaenda kuwa wakulima
wazuri na kuwanufaisha wengine” amesema Simba
Mkuu wa Chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole Bw. Sinani Simba wa tano kutoka kulia akisikiliza maelezo katika Hospitali ya Rufaa ya Wanyama nchini iliyopo SUA
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Maximilian Sarakikya,
amesema ushirikiano baina yao ya SUA utawasaidia kuwaleta wanafunzi wao kuja
kujifunza kwa vitendo, kuleta sampuli zao hususani za udongo kuja kuchunguzwa,
sambamba na kuomba ushirikiano na wataalamu wa SUA kuwaongezea maarifa hususani
kwenye tafiti.
“tumejifunza mengi sana kutoka kwa wenzetu SUA, wenzetu wametupita ngazi kubwa zaidi lakini tumejifunza mengi ambayo yatatusaidia baadae na katika ushirikiano wetu kuna mambo ambayo wenzetu watatushika mkono hususani Maktaba kwa Machapisho ya Kilimo na pia tumejionea jinsi wanafunzi wanavyotakiwa kusoma kwa vitendo” amesema Sarakikya
Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA
Dkt. Alex Matofali ameushukuru ugeni huo kwa kuzuru Kampasi hiyo, na kuwaahidi
kuyafanyia kazi yote waliyoyapendekeza hasa kupokea wanafunzi ili wajifunze kwa
vitendo.
0 Comments