NA, Hadija Zahoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kimefungua mafunzo ya siku mbili kwa watumishi wote ,kwa lengo la kuwakumbusha kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni taratibu na miongozo inayotolewa na serikali pamoja na Chuo katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu hayo chuoni hapo.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa SUA, yameanza tarehe 12 Aprili na kukamilika Aprili 13, 2022 katika ukumbi wa Multipurpose uliopo chuoni hapo, yanayowahusisha Wanataaluma wakiwemo Wakuu wa Idara na watumishi wote pamoja na Wasimamizi wa Miradi ya Utafiti SUA.
Akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Rafael Chibunda, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amesema Wakuu wa Idara zote, wanahusika moja kwa moja na mafunzo hayo kwa sababu wanasimamia na kuwezesha tafiti mbalimbali.
Amesema kwa kuonesha umuhimu wa mafunzo hayo, wamesimamisha masomo ndani ya siku hizo mbili kwa masomo ya asubuhi chuoni hapo, hivvo amewaomba wakuu hao wa idara kuwakumbusha wanataaluma wote kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanagusa mambo muhimu yakiwemo usimamizi na matumizi ya pesa za miradi,usimamizi na uendeshaji wa miradi ya utafiti chuoni, utunzaji wa kumbukumbu za miradi, utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotokana na utafiti , utekelezaji wa shughuli za ununuzi masuala ya afya na namna ya kuzingatia sheria za miongozo ya serikali na chuo katika mikataba husika ili kuepuka matatizo yatakayokikumba chuo na kufanya watatifi kushindwa kukamilisha kazi zao.
Aidha, Prof. Mwatawala amesema kuwa suala la kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo, litaisaidia chuo kuepuka hoja za kikaguzi zitakazoibuliwa na wakaguzi wa ndani na wale wa nje katika maeneo ya usimamizi wa miradi ya chuo na kukiingiza chuo katika matatizo makubwa ambayo yataleta doa litakaloichafua na kufunika kazi zote nzuri zitakazofanywa chuoni hapo.
‘‘Ndugu washiriki wa mafunzo kama nilivyoseam kufuata sheria,kanuni na taratibu kutatusaidia sana kuepuka hoja mbalimbali za kikaguzi na kukiingiza chuo katika matatizo makubwa, kwa sababu tunapokuwa na hoja hizo za kikaguzi hata tukitekeleza majukumu yetu mengine kwa ufanisi wa hali ya juu bado kunakuwa na doa kubwa , yani hilo doa linakuwa linafunika kazi zetu nzuri ambazo tumefanya hata kama tulifanya uzinduzi, uvumbuzi wa aina yoyote, lakini kwa kutofuata sheria na taratibu tunaweza kufunikwa na kuingia katika doa hilo’’. Amesema Prof. Mwatawala.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Prof. Loth Mulungu amesema kituo hicho kina hakikisha kinatoa matokeo ya tafiti yenye asili ya SUA kwa ajili ya kutatua matatizo katika jamii.
Ametolea mfano njia ya kutatua matizo ya panya kuharibu mazao hivyo wanafanya majaribio ya kutengeneza bidhaa kwa kutumia mkojo wa paka ili kuwafanya panya hao kuhisi uwepo wa paka na kupelekea kuogopa kuharibu mazao hayo.
0 Comments