Na: Gladness Mphuru
Wakazi wa Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla wameaswa kujenga utamaduni wa kuwahi kufika kwenye vituo vya Afya pale mtu anapopata dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu, ili kupata tiba kwa wakati kabla hajasababisha maambukizi ya ugonjwa huo kwa wengine.
PICHA MTANDAONI |
Hayo yamesemwa Machi 24, 2022 na Mratibu wa Huduma za Kifua Kikuu na Ukoma manispaa ya Morogoro, Dkt. Felista Rushimabahizi wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Kituo cha Afya cha Sabasaba kilichopo Manispaa ya Morogoro.
“Manispaa ya Morogoro tulianza kuiadhimisha siku hii tangu tarehe 21 siku ya Jumatatu kwa kutembelea maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa kuongeza uelewa juu ya ugonjwa huu kwa jamii, lakini pia tuliweza kupita kwenye baadhi ya vyombo vya habari ili kutoa elimu”, amesema Dkt. Felista.
Akitoa takwimu za wagonjwa wa Kifua Kikuu kwa kipindi cha mwaka mmoja Dkt. Felista amesema kwa manispaa ya Morogoro jumla ya watu waliobainika kuwa na maambukizi ni 884 huku Kituo cha Afya cha Sabasaba kikibaini wagonjwa 224.
“Kulingana na takwimu tulizonazo idadi ya wagonjwa ambao wanaibuliwa kuwa na Kifua Kikuu inaongezeka kwa sababu kwa mwaka 2020 takwimu za wagonjwa hao zilikuwa 864 na hii inatuonesha kwamba kwenye jamii bado tuna tatizo kubwa”, amesema Mratibu huyo.
Ameongeza kuwa mtu asipopata matibabu ya ugonjwa huu atapata madhara ya mwili kudhoofika, hivyo kupelekea kushindwa kufanya majukumu ya kila siku, uchumi kuathirika na kushindwa kujikimu na mwisho kupoteza maisha.
Aidha ametoa wito kwa jamii kuzingatia kanuni za kiafya na kujiepusha na misongamano isiyo ya lazima, ili kujiondoa katika hatari ya kuambukizwa magonjwa mbalimbali.
PICHA MTANDAONI |
0 Comments