Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amekagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi za kudumu za Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora unaoendelea katika Mji wa Serikali-Mtumba na kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Mhe. Jenista ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa ofisi hiyo
mara baada ya kufanya ukaguzi na kuielekeza Menejimenti ya ofisi yake
kuhakikisha inasimamia kikamilifu ili ofisi yake iwe ya kwanza kukamilisha
ujenzi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Jenista amesema, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora ilipata bahati ya kuwekwa kwa jiwe la uzinduzi wa
ujenzi wa ofisi za wizara zote katika Mji wa Serikali, hivyo ni vema kuilinda
heshima hiyo kwa kuwa wa kwanza kukamilisha ujenzi wa ofisi hizo.
“Nimeridhishwa na maendeleo ya ujenzi kwani kazi inaonekana
kuwa ni bora na hata taarifa ya Mshauri Elekezi inaeleza kuwa viwango vya
ujenzi vina ubora unaokubalika na unaoendana na thamani ya fedha inayotolewa na
Serikali.” Mhe. Jenista ameongeza.
Mhe. Jenista amempongeza Mkandarasi, Mshauri Elekezi na
Menejimenti ya ofisi yake kwa kuendelea kusimamia vizuri ujenzi wa ofisi hizo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ameungana na Mhe. Jenista Mhagama
kumpongeza Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Mshauri
Elekezi Watumishi Housing kwa kazi nzuri waliyoifanya ambayo imefikia hatua
inayoridhisha.
Dkt. Ndumbaro amewataka TBA na Watumishi Housing kuendelea na
kasi hiyo ya ujenzi ili kutekeleza maelekezo ya Mhe. Waziri ya kutaka ofisi
yake kuwa ya kwanza kukamilisha ujenzi pamoja na azma ya Serikali ya Awamu ya
Sita ya kutaka wizara zote kukamilisha ujenzi wa ofisi zake katika Mji wa
Serikali Mtumba.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa aliweka jiwe la uzinduzi wa ujenzi wa ofisi za wizara zote awamu ya
pili katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma tarehe 2 Desemba, 2021 kwenye
eneo linalojengwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
0 Comments