Na.Vedasto George.
Serikali imetakiwa kuweka mazingira wezeshi kwa vijana wanaomaliza Vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini kuweza kujiajiri kwenye Sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Utalii na Uvuvi ili waweze kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Taasisi binafsi ya VEDCOM Gaston Kaziri, wakati akizungumza na vijana zaidi ya 100 kutoka vyuo mbalimbali nchini kwenye Warsha ya kuwajengea uwezo wa kujiajiri kwenye Sekta ya Viwanda, Kilimo na Uvuvi inayofanyika Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo SUA.
Kaziri ameongeza kuwa changamoto kubwa inayowakwamisha vijana wengi nchini na kushindwa kujiajiri ni urasimu unaowekwa na Taasisi za fedha ambazo zina jukumu la kuwapatia mikopo yenye riba nafuu huku kisingizio kikiwa waliowengi hawana mali za kuwekea dhamana ili waweze kupata mikopo hiyo.
‘Lengo letu ambalo tunaliangalia kwa pamoja ni namna ambavyo tunaweza kusaidia vijana wetu wanaomaliza vyuo vya elimu ya juu kuweza kwenda kwenye ajira ya kujitegemea, kumekuwepo na utaratibu mzuri vyuo vyetu vinajitahidi kufanya kazi nzuri ya kuwafundisha vijana jinsi ya kujiajiri lakini sasa tunadhani kunatakiwa juhudi zaidi za kuweza kuwa na miradi mikakati ya kusaidia vijana hawa ambao wako vyuoni au wamemaliza vyuo lakini wangependa kuingia kwenye ajira ya kujitegemea”, amesema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mshauri wa mambo ya uwekezaji Taasisi binafsi ya VEDCOM Kilontsi Mporogomy amesema nafasi ya vijana katika kukuza pato la taifa ni kubwa hivyo ipo aja ya Serikali kushirikiana na Taasisi binafsi kuwakea mazingira mazuri vijana ambayo yatawasaidia kujiajiri na kuweza kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Hata hivyo Kilontsi amesema Serikali inapaswa kuwekeza zaidi kwenye Sekta ya Kilimo ili dhana ya Serikali ya Viwanda iweze kufikiwa kwa kujitosheleza kwenye malighafi ambazo zitasaidia kwenye viwanda hivyo.
Nao baadhi ya vijana ambao wameshiriki kwenye Warsha hiyo akiwemo Christo Zebedayo Msumeno kutoka Kituo Atamizi cha PASS AIC kilichopo mkoani Morogoro na Sada Jafari kutoka Chuo Kikuu Cha Mzumbe wamesema mafunzo hayo yanaenda kubadilisha mfumo wa maisha yao huku wakiongeza kuwa vijana wanatakiwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kuacha kutegemea ajira kutoka serikali.
“Sasa hivi dunia imebadilika vijana tukiweza kubadilika na tukaendana na Teknolojia inavyo kwenda basi hatuwezi kulia tena kwa kukosa ajira za serikali sasa hivi zipo fursa nyingi kwenye Kilimo, Ufugaji kote huko vijana bado hatujatumia vizuri fursa zilizopo huko, mafunzo haya sasa sisi tunaenda kuyabadili na kufanya kwa vitendo zaidi tunaamini tutafanikiwa”, amesema Msumeno.
0 Comments