SUAMEDIA

SUA yakusudia kufanya eneo lake la Bustani ya Mimea kuwa kivutio cha Utalii

 

Na: Amina Hezron

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Ndaki yake ya Misitu, Wanyama Pori na Utalii kimekusudia kufanya maboresho makubwa katika eneo lake la Bustani ya Mimea kuwa moja ya maeneo ya kisasa ya vivutio mkoani Morogoro kwa kuwa na bustani nzuri na ina eneo la ufugaji wa Wanyama Pori yaani Zoo.



Akizungumza na SUAMEDIA Rasi wa Ndaki hiyo Prof.  Suzana Augustino amesema kuwa Chuo kina mpango wa kuifanya bustani ya mimea yaani  botanic gadern kubadilika na tayari Chuo kimeshatenga pesa kwa ajili ya kazi hiyo .

“Tumewatumia wanafunzi wetu wa Misitu waweze kuainisha aina ya miti mbalimbali iliyopo, tuliwatumia  Wanafunzi wa Utalii waweze kuangalia vitu gani vinaweza kuwa kivutio humo na tunaweza kuvitangaza mtu aje, Wanafunzi wa Usimamizi wa Wanyama Pori  waweze kuangalia na wenyewe kuna Wanyama gani ambao ni kivutio lakini kikubwa tunao ndege “, amesema Prof. Suzana.

Ameongeza kuwa eneo hilo lililo mkabala na geti kuu la kuingia SUA linatarajiwa kupandwa maua na nyasi nzuri pamoja na baadhi ya  miti ya asili ambayo itapendezesha eneo hilo na kuvutia watu kulitumia kupiga picha na kupumzika.

Aidha Prof. Suzana amesema kuwa mwaka jana Serikali ilitoa ruhusu kuhusiana na mambo ya ufugaji wa Wanayama Pori hivyo kuna uwezekano wa kuzalishwa kwa Wanyama hao katika eneo hilo na  kisha wakifikisha umri mkubwa wakarudishwa porini kwenda kuishi huko ukizingatia kuna ukaribu wa eneo hilo na Hifadhi ya Taifa  ya Wanyama ya Mikumi.

“Kuna Wanyama wakubwa kama Simba hatuwezi tukazalisha hapa halafu tukamuacha akaja kuleta madhara, wanyama kama hao kuna taratibu zake tutawarudisha lakini vilevile  hata Twiga huwezi kusema tumezalisha Twiga wengi ngoja basi tuanze kula nyama  hapana”, alisema Prof. Suzana.

“Lakini kama mlivyosikia sheria iliyotoka pia sasa hivi inaturuhusu tuwe na mabucha ya Wanyama pori hivyo kwa maboresho ya botanic garden kulingana na mipango yake na mikakati tuliyoweka pengine  kuna uwezekano tutafikia tukaanza kama Chuo  na sisi tukawa na bucha ya nyama pori”, amesisitiza Rasi huyo wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii.


Post a Comment

0 Comments