SUAMEDIA

Jamii ya wafugaji nchini imeaswa kuwapatia chanjo mifugo yao

 

Flora Rugaimukamu

Jamii ya wafugaji nchini imeaswa kuhakikisha inawapatia chanjo mifugo yao kwa wakati pamoja na kuzingatia usafi wa mabanda  ili kuepukana na magonjwa na athari zinazoweza kujitokeza kwa Wanyama hao.




Akizungumza na SUAMEDIA Dkt. Veronica Massawe kutoka Hospitali ya Rufaa ya Wanyama iliyopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA  amesema kuna magonjwa mengi ambayo yanaweza kuwapata wanyama wafugwao majumbani ambayo mara nyingi hutegemeana  na msimu.

Dkt. Massawe amesema magonjwa ambayo yamekuwepo kwa wingi kwa wanyama hasa mbwa ni ugonjwa wa kuharisha na kutapika damu ambao kitaalam unafahamika kama Pavo ambao husababishwa na Virusi waonaweza kusambaa kwa haraka na kupelekea  kupoteza maisha endapo ugonjwa huo hutapatiwa huduma za matibabu kwa haraka.

Ametaja magonjwa mengine kuwa ni pamoja na magonjwa ya ngozi ambayo husababisha kupukutika kwa manyoya na kwamba ugonjwa huu unaweza kuzuilika kwa kuwapatia chanjo na kuogesha mifugo mara nyingi haswa paka na mbwa ambao wanakumbwa zaidi na kadhia hii.

"Katika Hospitali yetu tunapokea sana kesi ya ugonjwa wa kuharisha na kutapika damu kitaalam unaitwa  pavo ambao uwapata sana mbwa kwa kipindi hiki, lakini pia kuna ugonjwa wa masikio na ugonjwa wa ngozi kwa ng’ombe, mbuzi, nguruwe, na kondoo ambao hawawezi kuletwa hospitali lakini kuna madaktari ambao wanaweza kwenda hadi shambani kwa wafugaji kuwatibu", amesema Dkt. Massawe.

Aidha Dkt. huyo pia amewasihi wafugaji kuzingatia mambo muhimu ambayo wanaelekezwa na wataalam na kuwa waangalifu kwa wanyama wao na kuwataka kuwafikisha kwenye vituo vya matibabu au kuwasiliana na wataalamu wa mifugo pindi wanapoona dalili zozote za magonjwa.


Post a Comment

0 Comments