SUAMEDIA

Dkt. Nchemba: Serikali Kuziongezea Bajeti Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi

  Benny Mwaipaja, Dodoma


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameahidi kuwa Serikali, katika bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka 2022/2023, itaongeza bajeti katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili sekta hizo ziweze kuchangia kipato cha wananchi na Taifa kwa ujumla.



Dkt. Nchemba alitoa ahadi hiyo jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mashimba Ndaki, kujadili namna uwekezaji wa fedha za umma unaokusudiwa kufanywa kwenye Wizara yake unavyoweza kuongeza tija katika sekta ya mifugo na uvuvi.

Alisema kuwa sekta ya mifugo na uvuvi ikiwekewa miundombinu ya uhakika kwenye maeneo ya msingi yanayoweza kuonesha matokeo yanayopimika na ya haraka, inaweza kuleta mapinduzi makubwa ya kipato cha wananchi na hatimaye kuliwezesha Taifa kukuza uchumi wake.

Dkt. Nchemba alitolea mfano wa uendelezaji wa ranchi za Taifa, kukuza shughuli za uvuvi kwa kuwekeza vitendea kazi vya uhakika yakiwemo maboti ya uvuvi kutaiweza nchi kuzalisha mazao ya mifugo na uvuvi kwa wingi na kuuza nje ya nchi ili kupata fedha za kigeni.

Alimshauri Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuelekeza rasilimali fedha watakazopatiwa kwenye maeneo yenye viwanda vya kuchakata nyama na maziwa ili kuongeza mnyororo wa thamani pamoja na kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwenye viwanda hivyo.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru alisisitiza kuwa malengo ya kutaka kuipatia Wizara hiyo fedha nyingi zaidi ni kuonesha kuwa hivi sasa Serikali inataka kuona kuwa fedha hizo zinakuwa ni uwekezaji badala ya kuwa fedha za matumizi ya kawaida.

Alisema kuwa sekta muhimu kama kilimo, mifugo na uvuvi zikiboreshwa, zitakuwa na matokeo makubwa na chanya kiuchumi na kijamii kwa sababu zitakuza ajira, zitaongeza wigo wa mauzo nje ya nchi na kuwaondolea wananchi umasikini wa kipato pamoja na kuiwezesha nchi kulipa deni lake la Taifa.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mashimba Ndaki, alieleza kuwa fedha zitakazotolewa na Serikali zitaelekezwa katika maeneo ya kuboresha shughuli za uvuvi ambapo wanatarajia kununua maboti ya uvuvi 348, kujenga mialo na masoko ya kuuzia samaki kwenye maeneo ya kimkakati.

Katika eneo la Mifugo, Mheshimiwa Mashimba alieleza kuwa nguvu zaidi zitaelekezwa kwenye maeneo ya kuboresha mifugo kupitia ranchi za taifa na makundi maalumu ya wafugaji, kuimarisha huduma za ugani na kunenepesha mifugo ili iwe na tija ambapo alisema kuwa sekta hizo mbili, kwa kuanzia, zitahitaji zaidi ya dola za Marekani milioni 105, sawa na takribani shilingi bilioni 270.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Sekta ya Mifugo, Bw. Mbaraka Stambuli, alisema kuwa eneo lingine litakalopewa kipaumbele ni kukabiliana na magonjwa yanayoathiri mifugo ili kuiwezesha sekta hiyo kuzalisha nyama na maziwa, yanayokidhi viwango vya ubora vya kimataifa.

Post a Comment

0 Comments