NA.AYOUB MWIGUNE
Wafugaji nchini wametakiwa kuwashirikisha wataalam wa mifugo kwa lengo la kupata elimu na njia bora za ufugaji ili waweze kuongeza kipato chao pamoja na Taifa kwa ujumla .
Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Shamba la Mifugo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Jonatas Venance Karol wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu umuhimu wa kuwatumia wataalam wa mifugo katika masuala ya ufugaji.
Bw. Venance amesema unapofuga ng’ombe lazima utambue kwamba ili uweze kupata faida kubwa huna budi kuwashirikisha wataalam hasa kutoka SUA ambao watakusaidia kupata elimu ya njia bora za ufugaji ambazo zitakuwezesha kupata kipato na kuwa na mifugo yenye afya bora.
Aidha amesema miongoni mwa changamoto zinazosababisha wafugaji wengi kushindwa kuwapa mifugo yao lishe bora ni pamoja na kutozingatia suala la lishe Katika mifugo yao na kutowahusisha wataalamu wa mifugo.
“Mfugaji anapofuga lazima awatafute wataalam ili kile anachokifanya kiwe na matokeo chanya kuanzia kwenye ujenzi wa Banda, namna ya kuzuia magonjwa na namna ya uzalishaji ”, alisema Bw. Venance.
Akielezea kuhusu lishe ya ng'ombe hasa katika kipindi hiki ambapo kumekuwa na mvua nyingi amesema majani yamekuwa mengi katika mashamba na yanakuwa na majimaji ambapo yanakosa virutubisho hivyo mkulima anatakiwa pamoja na kuwapa majani ya kawaida lazima ahakikishe wanaporudi jioni anawapa majani makavu ili aweze kupata maziwa mengi.
0 Comments