Na.Vedasto George.
Utafiti uliofanywa katika mikoa ya Morogoro, Rukwa, Mbeya na Iringa umebaini kuwa asilimia 60 hadi 70 ya udongo katika mikoa hiyo umepoteza virutubisho vyake na kusababisha wakulima wa mazao ya mahindi, alizeti, viazi na mpunga kutopata mazao yenye ubora na tija na kusababisha familia nyingi kuendelea kuwa masikini.
![]() |
Picha Mtandaoni |
Hayo yamebainishwa na Mtafiti wa Udongo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania -TARI Uyole na Kiongozi wa Mradi wa Uboreshaji wa Kilimo Bora kwa Wakulima FREDRICK MLOWE ambapo amesema utafiti huo umefanyika katika vijiji 400 vya mikoa hiyo na kubaini virutubisho vya msingi katika udongo vimepotea kutokana na matumizi mabaya ya ardhi.
“Udongo wa maeneo yote tuliyopita umechoka, ukosefu wa kirutubisho cha zinki peke yake katika udongo kwenye kilimo cha mpunga unaweza ukapelekea mkulima kukosa mavuno kwa asilimia 30 mpaka 35 lakini uwepo wa upungufu wa kirutubisho cha Sulpha kwenye udongo mkulima anaweza kukosa mavuno kwa asilimia 70, kwa hiyo ardhi yetu katika mikoa hii imechoka sana”, amesema Mtafiti huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Kilimo TARI Uyole Dkt.TULOLE LUGENDO amesema licha ya udongo kutokuwa na virutubisho vya kutosha lakini bado mazao mengine yanaweza kulimwa katika mikoa hiyo.
“Kitu kingine ambacho tumekigundua ni kwamba kuna uwezekano wa kuanzisha mazao mapya ambayo yalikuwa hayajazoeleka, mazao kama michikichi, kokoa na makadamia yanaweza kulimwa na wakulima wakapata faidia kubwa”, amesema Dkt. Lugendo.
Mhandisi JUMA MDEKE Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi kutoka Wizara ya Kilimo amesema Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa kilimo nchini ili kukifanya kilimo kiweze kuwanufaisha wakulima na taifa kwa ujumla.
“Sisi watu wa sera tunasema ili upate tija ni lazima kufahamu Afya ya udongo ya maeneo husika basi sisi kama wizara tutahakikisha matokeo haya yaliyopatikana kwenye utafiti huu yanatumika kwa sababu dhamila yetu kama wizara ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 kuwepo na food security na food security haiwezi kuwepo kama wakulima wetu wataendelea kulima kizamani”, amesema Mhandisi MDEKE
0 Comments