Mjumbe wa Bodi ya Shirikisho la Mageuzi ya Kijani Afrika (AGRA) na Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amepongeza jitahada kubwa zinazofanywa na AGRA nchini Tanzania katika kukuza kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
Dkt. Kikwete ameyasema
hayo Mkoani Iringa katika siku yake ya kwanza ya ziara ya ukaguzi wa miradi ya
kilimo inayofadhiliwa na AGRA ambapo amepata fursa ya kuwatembelea wachakataji
wa mazao ya kilimo na wauzaji wa pembejeo na kujionea namna ambavyo wadau hao
wa kilimo wamesaidia kujiongezea kipato na kutengeneza fursa nyingi za
Ajira kwa wakulima wengi na hivyo kuwa
kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya Kilimo.
“Mimi ni Mjumbe wa
Kamati ya Mipango ya AGRA, tulikubaliana kwenye Bodi kwamba wajumbe tupite
kukagua miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na AGRA, nimefarijika kuona
miradi mingi ni mizuri na imeleta athari chanya kwa wakulima wetu na
wachakataji wa mazao ya kilimo, hii itasaidia sana kukuza sekta ya kilimo na
kukuza uchumi wa Nchi yetu”, alisema Dkt. Kikwete
Naye Naibu Waziri wa
Kilimo Mh. Anthony Mavunde ameishukuru
AGRA kwa kazi kubwa inayofanya katika kumjengea uwezo mkulima wa nchi hii na
kuhakikisha kwamba zao la kilimo linaongezewa thamani jambo ambalo ndio muelekeo
wa serikali na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo ili malengo ya nchi
kupitia kilimo yaweze kutimia.
Katika ziara hiyo ya
siku 5 Dkt. Kikwete ameongozana na Makamu wa Rais wa AGRA Bi. Aggie Asimwe Konde pamoja na
wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo.
0 Comments