SUAMEDIA

SUA hongera kwa kuwapa watumishi mafunzo ya uadilifu- TAKUKURU Arusha

 

Gerald Lwomile

 Arusha

 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Arusha imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo ya uadilifu kazini chini ya Kamati yake ya Kudhibiti Uadilifu (KKU) jambo ambalo linaweza kuleta maendeleo makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla


Afisa wa TAKUKURU mkoani Arusha Bi. Jacqueline Kapile aliyesimama akiongea na watumishi wa SUA Kampasi ya Olmotonyi

Pongezi hizo zimetolewa na Afisa wa TAKUKURU mkoani Arusha Bi. Jacqueline Kapile Februari 23, 2022 wakati akitoa mafunzo ya maadili ambayo ni nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Kampasi ya Olmotonyi

Akizungumza katika mafunzo hayo Bi. Kapile amesema pamoja na SUA kutoa fursa hiyo lakini ni muhimu kwa watumishi hao kujenga jamii yenye uadilifu kwa kuhakikisha wanajenga maadili toka nyumbani kwani mzazi anao wajibu mkubwa wa kujenga maadili ya mtoto lakini pia na yeye kuwa na maadili mema

“Kama wazazi tunao wajibu mkubwa kuhakikisha tunawajenga watoto wetu katika misingi ya maadili, unakuta mtoto ili atumwe anauliza utanipa shilingi ngapi hapana haya si maadili kwa hiyo tuwakumbushe Watoto kuwa nimekutuma kama mzazi”amesema Kipile

Aidha Bi. Kapile amesema watumishi wa Serikali au Umma wanapotamani kuishi maisha ya anasa ambayo hayalingani na kipato chao halisi, huwa mwanzo wa kujihusisha na rushwa.

 

“Mtumishi huyu huanza kubuni mbinu itakayompatia fedha kwa haraka, matokeo yake huangukia katika vishawishi vya kupindisha haki na maadili ilimradi kaahidiwa  au kupewa hongo” amesema Bi. Kapile

 

Akizungumza katika kikao hicho Meneja wa Kampasi ya Olmotonyi Bw. Said Sallum Kiparu amesema katika kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji ni muhimu kuhakikisha kila mtumishi anafanya kazi kwa bidii na kuleta ufanisi katika eneo la kazi


Meneja wa Kampasi ya Olmotonyi Said Sallum Kiparu aliyekaa katikakati akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wajumbe wa KKU na watumishi wa SUA Kampasi ya Olmotonyi

Amesema jambo la uaminifu katika kazi ni jambo la msingi na linaweza kusaidia kuondoa mgongano wa kimaslahi kwa mtumishi na kusababisha kuwepo kwa maendeleo makubwa katika jamii

Akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti Uadilifu SUA Prof. Christopher Mahonge amesema wafanyakazi wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanachangia katika maendeleo ya taifa kwa kufanya kazi kwa bidii

Amesema kamati yake imefungua milango kwa kila mtumishi katika taasisi hiyo kutoa taarifa za ukiukwaji wa maadili na kuwa mtoa taarifa atalindwa kutokana na sheria, kanuni na miongozo ya utoaji taarifa.

Post a Comment

0 Comments