SUAMEDIA

Malipo ya Ushuru wa Maegesho sasa ni kidigitali

 Na Farida Mkongwe

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA mkoa wa Morogoro itaanza kukusanya ushuru wa maegesho ya vyombo vya moto kwa njia ya Kielekitroniki kama njia moja wapo ya kukabiliana na upotevu wa fedha unaotokana na mfumo kwa sasa.


Mtaalam wa Mifumo ya TEHAMA-TARURA akitoa maelekezo kuhusu mfumo mpya wa ukusanyi ushuru katika manispaa ya Morogoro


Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Morogoro Mtalaam wa Mifumo ya TEHAMA kutoka TARURA Bw. Shadrack Mahenge amesema mfumo huo wa kidigitali utaanza kutumika kuanzia tarehe 1 mwezi Machi, 2022.

Bw. Mahenge amezitaja faida nyingine za mfumo huo utakaoanza kutumika mwezi ujao kuwa ni kuongezeka kwa mapato ya Serikali, kudhibiti wakwepaji ushuru, kuwezesha utengenezaji wa taarifa za mapato kwa haraka pamoja na kuwawezesha watumiaji wa vyombo vya moto kuwa na muda wa kutosha wa kufanya malipo.

“Kuna baadhi ya madereva walikuwa wanakwepa kulipa ushuru hata baada ya kuwekewa Ankara za malipo, pia kulikuwa na usumbufu wa kutafuta chenji na hivyo kupoteza muda mwingi, lakini pia wengine sio waaminifu mnajua tena pesa ukishaishika mkononi lakini sasa matatizo hayo yanaenda kumalizika”, amesema Bw. Mahenge. 

Kwa upande wake Mwanasheria wa TARURA mkoa wa Morogoro Tausi Madebo amewataka watumiaji wa maegesho ya vyombo vya moto kuzingatia sheria na Kanuni na kufanya malipo ndani ya siku 14 tangu wanapowekewa ankara za malipo ili kuepuka ulipaji wa faini.

“Endapo mmiliki wa chombo cha usafiri atashindwa kulipa ushuru wa maegesho kwa mujibu wa kanuni ya (2) baada ya siku 14 basi mmiliki huyo atakuwa amekaidi na atawajibika kulipa faini ya sh. 10,000/= pamoja na ushuru aliopaswa kulipa”, amesema Mwanasheria huyo.

Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro wakifuatilia kwa makini maelekezo ya namna mfumo huo utakavyofanya kazi

Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro wakifuatilia kwa makini maelekezo ya namna mfumo huo utakavyofanya kazi


Post a Comment

0 Comments