SUAMEDIA

Redd+ yazinduliwa, Taasisi kujengewa uwezo kupunguza Hewa Ukaa

 

Na Farida Mkongwe

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga amezindua rasmi Mradi wa Kujenga Uwezo wa Taasisi ili Kupunguza Hewa Ukaa inayosababishwa na ukataji miti na uharibifu wa misitu unaojulikana kwa jina la REDD+ 

Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kufanya uzinduzi wa Mradi wa REDD+

Akizindua Mradi huo ambao unafadhiliwa na Serikali ya Norway Bi. Mary amesema kimsingi mradi wa REDD+ utasaidia kuharakisha zoezi la kuhifadhi misitu kwa njia mbalimbali ikiwemo upandaji wa miti na kuhifadhi vyanzo vya maji.

“Kwa hiyo Mradi huu ambao tumeuzindua utatusaidia kuwa na Mikakati endelevu ya kutunza na kuhifadhi misitu, tuelewe mabadiliko ya tabianchi yanaathiri dunia nzima lakini kwa sisi bado tunaweza kuirudisha ardhi kama ilivyokuwa kwa kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji ili kusaidia na kwingine ambako kumeshaharibika”, amesema Katibu huyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba amesema Mradi wa REDD+ utasaidia sana kwani kwa sasa takribani wastani wa hekta 469,000 zinakatwa kwenye misitu hapa nchini kwa ajili ya matumizi mbalimbali

“Kasi hii ya ukataji miti sio nzuri kwa maendeleo au mustakabali wa mazingira yetu, sasa tunakwenda kutafuta nishati mbadala, tunataka kutumia kilimo ambacho hakitumii maji mengi, tutahakikisha wafugaji wanapata malisho na maji kwenye maeneo yaliyoendelezwa badala ya kutumia vyanzo vya maji”, amesisitiza Dkt. Komba

Naye Mratibu wa Program wa Shirika la Mazingira IUCN Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini Charles Oluchina amewaomba watanzania kutoa ushirikiano kwa sababu Tanzania ni nchi muhimu sana kwenye kilimo.

“Mchango wa kilimo kwa Tanzania, Afrika mashariki na Kusini ni mkubwa sana, mazao yanayotokea Tanzania yanalisha hadi Angola, Kusini Sudan hadi sehemu za Kenya”, amesema Mratibu huyo. 

Mradi wa REDD+ awamu ya pili umezinduliwa Februari 23, 2022 ukiwa na lengo la kuiwezesha Tanzania kuwa tayari katika utekelezaji wa Makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi (Paris Agreement) ili kunufaika na biashara ya hewa ukaa ifikapo 2022.





Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga akitoa hotuba ya uzinduzi wa Mradi REDD+ mjini Morogoro



Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wengine waliohudhuria kwenye uzinduzi huo












 

Post a Comment

0 Comments