Hadija Zahoro
Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza ICE iliyopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, imesema inafanya jitihada kubwa kuhakikisha teknolojia, elimu na bunifu ambazo zimezalishwa chuoni hapo zinawafikia wakulima wadogo ili kukidhi mahitaji yao pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.
Akizungumza na SUAMEDIA Mkuu Kitengo cha Ugani Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza SUA (ICE) Dkt. Innocent Babili amesema Taasisi hiyo hufanya kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine zilizopo Chuoni hapo ikiwemo SUAMEDIA na tovuti mbalimbali ili kuifikia jamii kwa sababu chuo cha SUA ni kikubwa.
Amesema njia nyingine wanayotumia kuwafikia Wakulima wadogo ni kuandaa Maonesho mbalimbali yakiwemo ya Nanenane, Maonesho wakati wa Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine pamoja na Maonesho ya Kilimo ambayo mara ya mwisho yalifanyika mwishoni mwa mwaka 2021 jijini Mwanza kama sehemu ya Kumbukizi ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.
Dkt. Babili amesema mafunzo mengi ya muda mfupi yanayotolewa na ICE huwa yanawalenga wakulima hao, huku akitolea mfano Mafunzo ya Ufugaji wa Samaki, Mafunzo ya Bustani, kubebesha Miche ya Matunda na mafunzo mengineyo ambayo huwa na tija kwa wakulima.
‘‘Ile tu kuwa na mafunzo ya kilimo yanayowalenga wao, ni kuonesha kwamba inawajali na kwa SUA wakulima wana hadhi kubwa lakini pia kuna mafunzo ya bustani na tumeshaendesha kwa watu tofauti tofauti, kubebesha miche ya matunda ili watu waweze kupata mavuno kwa muda mfupi ukiachana na yale yanayochukua muda mrefu’’,ameongeza Dkt. Babili
Akizungumzia mafanikio ya mafunzo hayo Dkt. Babili amesema Chuo kimepokea mrejesho mzuri kutoka kwa wadau mbalimbali nchini ambao wamepata mafunzo na kuyatekeleza kwa vitendo kwamba wamefanikiwa kuboresha sehemu walizokuwa wanakwama na wengine kufikia hadi hatua ya kujiajiri wenyewe.
0 Comments